Usawa wa kijinsia sio kukandamiza kundi fulani-Dkt.Jingu

DODOMA-Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt.John Jingu amesema, dhana ya usawa wa kijinsia sio kukandamiza jinsi yoyote bali kuweka mifumo mizuri itakayosaidia kuwa na fursa sawa kwa jinsi zote na nyanja mbalimbali.
Katibu Mkuu Dkt. Jingu ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kikaokazi cha siku moja kilicho wakutanisha Maafisa Viungo wa Madawati ya Kijinsia kutoka Wizara za Kisekta pamoja na Wadau wa Maendeleo walipokutana jijini Dodoma leo Agosti 15, 2023.

Amesema,baadhi ya watu hawaelewi dhana usawa wa kijinsia, wengine wanahusisha usawa na kijinsia na ubaguzi au kulinda kundi moja ndani ya jamii dhana ambayo sio kweli.
Aidha, Dkt. Jingu amewataka Maafisa hao kutoka Wizara za kisekta kuwa chachu ya kuwabadilisha watu walio wengi wanaodhani usawa wa kijinsia ni kuikandamiza jinsi Moja ili waweze kuelewa dhana hiyo maana yake na inavyosaidia kuleta maendeleo jumuishi katika jamii.

Dkt. Jingu ameongeza kuwa, Maafisa wa Madawati hao wasingoje kuwasilisha taarifa pekee kama ilivyo sasa badala yake waongeze ubunifu ili shughuli wanazofanya ziweze kufahamika lakini pia kuwa na mashiko hasa kwenye kutoa elimu sahihi kuhusu usawa wa kijinsia wakianza na ofisi zao na kwa jamii.
"Ukiwasha taa na kuiweka chini ya uvungu huwezi kupata nuru, lakini ukiweka juu, nuru itaonekana hivyo hivyo kwenye majukumu yenu lazima mzingatie hili" amesema Dkt. Jingu

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Badru Abdunur amesema kuwa vikao vya wataalam hao hukutana kila robo mwaka kwa lengo la kupokea taarifa za masuala ya jinsia na kuweka mikakati ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao hivyo katika kikao hicho watajadiliana zaidi kuwa na mbinu bunifu katika kuhakikisha dhana ya usawa wa kijinsia inaeleweka kwa jamii.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa UN Women kwenye mkutano huo, Usu Malya ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa hatua inayopiga wakati wa kushughulikia masuala ya jinsia hasa kuhakikisha inaratibu madawati ya jinsia ndani ya wizara za kisekta ili kuweka nguvu katika masuala ya kijinsia yanazingatiwa hasa kwa upangaji wa mipango na bajeti mbalimbali za maendeleo.

Kikao kazi hicho cha siku moja, kinapokea taarifa za utekelezaji wa sekta na wadau kuhusu usawa wa kijinsia kwa kipindi Januari hadi Juni, 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news