Maandalizi ya African Football League

DAR ES SALAAM-Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amepokea ugeni wa timu ya wataalam wa African Football League chini ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ili kuanza maandalizi ya ufunguzi rasmi wa mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Oktoba 20, 2023 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya ziara ya ukaguzi wa maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati ili kuendana miongozo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Yakubu amesema mazungumzo yao yalijikita zaidi kuangalia ubora wa Uwanja na maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati.

“Mazungumzo yetu yalijikita zaidi pamoja na ziara ya uwanja kuangalia ubora wa uwanja na maeneo ambayo tunaenda kuyafanyia ukarabati na mahitaji yao kwa ajili ya mechi ya ufunguzi ambayo kwa bara zima la Afrika itafanyika hapa katika uwanja huu wa Benjamin Mkapa,”amesema Katibu Mkuu, Yakubu.

Mashindano ya African Football League yanatarajiwa kuwa na manufaa mengi kiuchumi hapa nchini kwa kuwaleta wageni mashuhuri takriban 400 ambao watashiriki wakiwemo viongozi wa juu wa CAF na FIFA.

Katibu Mkuu, Yakubu amesema wizara hiyo tayari imeshaingia mkataba na mkandarasi mkandarasi wa ukarabati huo Beijing Construction Engineering Group Co., Ltd. (BCEG) na kusisitiza kuwa mkandarasi huyo amekabidhiwa rasmi uwanja ili aendelee na majukumu yake ya ukarabati.

Ukarabati wa awali utajumuisha masuala mbalimbali ambayo CAF wanahitaji yafanyiwe kazi mapema, baadhi yanagharamiwa ikiwa ni sehemu ya mkataba na baadhi ni gharama inayotolewa na CAF kwa ajili ya mechi hiyo ya ufunguzi ambayo itafanyika nchini.

Kwa hivi sasa mpaka Oktoba 20, 2023 hakutakuwa na mechi nyingine itakayochezwa kwenye uwanja huu wa Benjamin Mkapa ili kupisha maandalizi kwa sababu miongoni mwa vitu watakavyofanya African Football League ni pamoja na kufumua eneo la kuchezea mpira kwa gharama zao na watalirejesha kwenye hali ambayo unachezeka mpira.Michuano hiyo inashirikisha vilabu nane kote barani Afrika Simba ikiwemo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news