Musoma Vijijini waendelea kutabasamu

NA FRESHA KINASA

WAKAZI Katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha ujenzi wa hospitali ya halmashauri hiyo, (Musoma DC), ambapo hivi sasa watapata huduma karibu na hivyo kuondokana na changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

Wameyasema hayo Agosti 9, 2023 wakati wa uzinduzi wa utoaji wa huduma mbalimbali za afya uliofanyika katika Kitongoji cha Kwikonero Kijiji cha Sugiti Kata ya Suguti mahali iliyojengwa hospitali hiyo.

Ambapo viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi akiwemo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Vijijini, Denis Ekwabi, Viongozi wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Halfan Haule, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospter Muhongo na Wananchi kwa ujumla wamehudhuria.

Naomy Bwire mkazi wa Suguti amesema,badala ya kusafiri umbali mrefu kwenda Musoma Mjini kupata matibabu mgonjwa anapopewa rufaa kutoka kwenye vituo vya afya na zahanati hivi sasa matibabu hayo watayapata karibu na maeneo yao na hivyo kuokoa gharama za usafiri.

Jesca Paulo amesema kuwa, kina mama wajawazito ambao walikuwa wakipewa rufaa ya kwenda Musoma Mjini kwa upasuaji na wakati mwingine kuwa katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na umbali kwa sasa wameondokana na kadhia hiyo Jambo ambalo amesema Serikali inapaswa kupongezwa.

"Namshukuru Rais wangu Samia Suluhu Hassan na Mbunge Prof. Muhongo kwa hakika wanaupiga mwingi sana, mwanzoni tulidhani hospitali hii isingekamilika, lakini imejengwa kwa kasi na kukamilika lazima tuwapongeze viongozi wetu kujali afya za watanzania. 
 
"Badala ya kwenda Musoma Mjini umbali wa kilomita 90 tumepata Hospitali ya Wilaya ambayo imejengwa kisasa kabisa na huduma zote tutapata,"amesema Fabian Mafuru.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya wa Musoma, Dkt. Halfan Haule akizindua utoaji wa huduma mbalimbali za afya kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma amesema kuwa, Serikali imeshaleta vifaa vya tiba na wataalamu mbalimbali wakiwemo madaktari, wataalamu wa maabara, Wauguzi, Maafisa afya, Afisa mazingira, Afisa Ustawi wa Jamii wataalamu wa matengenezo ya vifaa vya afya.

Dkt.Haule amesema kuwa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kusudi washiriki kikamilifu kufanya shughuli za uzalishaji kwa ajili ya kuchochea maendeleo yao na maendeleo ya uchumi wa nchi. Huku akisema kuwa wataalamu hao wapo tayari kuwahudumia wananchi.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof.Sospeter Muhongo ameishukuru Serikali kwa kusema imekuwa ikifanya kwa ufanisi kile ambacho Wananchi wanahotaji Jambo ambalo linawapa furaha wananachi na kuzidi kuiamini serikali.

"Tujipe hongera, kwani yametia, lazima tuishukuru Serikali yetu kwa dhati inatupenda sana tukiomba tunapewa na mgao wa aina yoyote ukitolewa tumo."amesema Prof. Muhongo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini imesema kuwa, "Hospitali hii yenye kutoa huduma za afya kwa kiwango cha hadhi ya Hospitali ya Wilaya, hadi sasa Serikali imeishatoa shilingi bilioni 3.49 kwa ajili ya ujenzi, na shilingi milioni 600 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa.Majengo muhimu tisa yamekamilika, na majengo mengine sita yanaendelea kujengwa likiwemo jengo la kufulia."

"Hospitali ina vifaa vya kisasa, vikimemo Digital X-ray, Ultrasound na Mitambo ya kutengeneza Oxygen ambayo inapelekwa sehemu ya matibabu kupitia mtandao wa paipu. Mitungi ya Oxygen ipo ikiwa ni kwa matumizi ya dharura au kusaidia mahitaji ya hospitali nyingine, vituo vya afya na zahanati."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news