Ni fainali ya moto, hapa Simba SC vs Yanga huku Azam FC vs Singida Fountain Gate FC

NA DIRAMAKINI

VIGOGO wa soka Tanzania wapo katika maandalizi ya mwisho kuelekea Fainali ya Ngao ya Jamii ndani ya dimba la Mkwakwani jijini Tanga.

Pande hizo zinatarajiwa kukutana Agosti 13, 2023 majira ya saa 1:00 usiku wakitanguliwa na Azam FC dhidi ya Singida Fountain Gate FC ambao wanasaka nafasi ya tatu, mtanange wao utapigwa majira ya saa 9:00 alasiri dimbani hapo.

Fainali hiyo ambayo inawakutanisha Yanga SC dhidi ya watani zao Simba SC, Yanga SC walikuwa wa kwanza kutangulia fainali Agosti 9,2023 baada ya kuitwanga Azam FC mabao 2-0.

Ni kupitia mtanange uliopigwa katika Dimba la Mkwakwani jijini Tanga ambapo Yanga SC ambao ni mabingwa watetezi wa ngao hiyo, waling'ara kupitia mabao ya Stephane Aziz Ki dakika ya 85 na Clement John Mzize dakika ya 89.

Aziz Ki na Mzize walipeleka furaha hiyo Jangwani baada ya kutokea benchi kwa pamoja dakika ya 62, Aziz Ki akichukua nafasi za Crispin Ngushi na Mzize nafasi ya Farid Mussa wakati wa mtanange huo.

Kwa upande wa Klabu ya Simba ilifanikiwa kutinga fainali Agosti 10, 2023 baada ya kuifunga Singida Fountain Gate kwa mikwaju ya penati 4-2.

Ulikuwa kati ya michezo ya awali katika maandalizi kuelekea msimu wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara 2023/2024 ambao ulionesha ushindani mkubwa, katika dimba la Mkwakwani baada ya sare ya bila kufungana katika muda wa kawaida.

Mchezo ulianza kwa kasi huku pande zote zikishambuliana kwa zamu, lakini umakini kwenye eneo la mwisho ulikosekana hasa kwa Simba SC.

Aidha, kipindi cha pili, Simba SC walirudi kwa kasi na kuliandama lango la Singida huku Singida wakionekana kukaa nyuma na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza, lakini safu ya Wekundu hao ya ulinzi ilikuwa imara.

Mlinzi wa kati Henock Inonga alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumizwa bega na mshambuliaji Medie Kagere.Penati za Simba SC ziLIfungwa na Luis Miquissone, Saido Ntibazonkiza, Mzamiru Yassin na Moses Phiri.

Kwa upande wa Singida penati zao zlifungwa na Tchakei na Duke Abuya huku Aziz Andambwile na Yusuph Kagoma wakikosa.

Singida Fountain Gate na Azam FC zitamenyana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu. Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) viingilio vya katika fainali hiyo vimegawanyika makundi mawili.

Viingilio vya kundi la kwanza kwa maana ya VIP B ni shilingi 30,000 huku kwa upande wa kundi la pili viingilio kwa mzunguko ni shilingi 20,000.

Awali,Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ alisema, walikuwa bora zaidi ya Singida Fountain Gate na walistahili kushinda ingawa ilikuwa kwa penati.

Robertinho alisema, walikuwa bora maeneo mengi wakitawala sehemu kubwa ya mchezo huku Singida wakicheza mpira wa kasi na kushambulia kwa kushtukiza.

Pia, kocha huyo aliwasifia wachezaji wake kwa kazi kubwa waliyofanya huku akimvulia kofia mlinda mlango, Ally Salim kwa kufanikiwa kuokoa penati ya kwanza.

“Lazima nikubali tumepata upinzani mkubwa, Singida wamecheza vizuri, lakini sisi tulikuwa bora zaidi yao. Naweza kusema timu bora imeshinda ndani ya uwanja,”alisema Robertinho.

Akizungumzia mchezo wa fainali dhidi ya Yanga siku ya Jumapili, Robertinho alisema, utakuwa mgumu lakini wapo tayari kuwakabili.“Itakuwa mechi ngumu, ni Derby na siku zote inakuwa hivyo." Tuna siku siku mbili za kujiandaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news