Niwapongeze kwa mawazo haya ya mageuzi-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amehimiza ushirikiano wa kiutendaji baina ya taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ili kuendeleza mageuzi ya uchumi na uwekezaji.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Tanzania, Mhe.Prof. Kitila Mkumbo, baada ya kumaliza mazungumzo na kujitambulisha alipofika Ikulu jijini Zanzibar na ujumbe wake, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu.(Picha na Ikulu). 

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Agosti 5,2023 Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo na ujumbe wake wa watu 20 waliofika kujitambulisha.

Alisema, SMZ na SMT wana ushirikiano mkubwa kwenye utendaji wa taasisi zao na kueleza, mara kadhaa taasisi ya Hazina ya Zanzibar imekuwa ikipata ushirikiano mzuri na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na TIC pamoja na taasisi nyingine za pande mbili hizo za Muungano hushirikiana katika kuboresha maendeleo kwa ustawi wa uchumi wa taifa la Tanzania na watu wake.

Rais Dkt.Mwinyi pia alitumia fursa hiyo kuwapongeza na kuushukuru ujumbe huo kwa utayari wao kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mawazo ya mageuzi yanayolenga kujenga uchumi wa wananchi wa pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni kupitia ushirikiano uliopo baina ya tasisi za serikali mbili hizo, zikiwemo Mamlaka ya Bandari, Ofisi ya Msajili Hazina, Mamlaka za Uwekezaji pamoja na Tume ya Mipango ya Taifa.

“Niwapongeze kwa mawazo haya ya mageuzi, ni vizuri mara zote tuwe kunafikiria kujenga uchumi wetu kupitia taasisi zetu,”alibainisha Rais Dkt.Mwinyi.

Akiizungumzia bandari Jumuishi ya Mangapwaji, Rais Dkt.Mwinyi, alimueleza Waziri huyo kwamba SMZ imepania kuleta mageuzi makubwa ya uchumi kupitia bandari hiyo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alisema, kutokana na maumbile ya kisiwa cha Zanzibar kilivyo, inakusudiwa kujumuisha shughuli zote za bandari mbali na kupakia na kushushia abiria na mizigo, lakini kuruhusu meli mbalimbali za kimataifa zitakazoleta mageuzi makubwa ya biashara, uwekezaji na kuimarisha uchumi wa buluu.

Naye Waziri Prof.Mkumbo alimuahidi Rais Dkt.Mwinyi ushirikiano wa hali ya juu katika kuujenga uchumi wa nchi hasa kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar wamejipanga kuleta mabadiliko makubwa ya uchumi.

Alisema, mbali na mambo mengine lakini kupitia mradi wa Bagamoyo, ujio wa Zanzibar umewaletea tija na ufanisi mkubwa kwenye utendaji wao hasa kwa taasisi wanazoshirikiana nazo kiutendaji kwani watajifunza mengi kupitia bandari jumishi ya Mangapwani pamoja na taasisi nyingine wanazoshirikiana nazo kiutendaji.

Ujumbe ulioongozana na Waziri Prof. Kitila umemjumuisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, Msajili wa Hazina Bara, Nehemia Mchechu, Katibu wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru, Mkurugenzi Mkuu EPZA, Charles Itembe, Mkurugenzi Mkuu, TIC Gilead Teri na Mkurugenzi wa Miundombinu TPA, Dkt.Hussein Lufunyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news