Hii hapa, Ratiba ya shughuli za Kamati za Kudumu za Bunge kwa kipindi cha Agosti 7 hadi 25,2023

1.0 UTANGULIZI
 
Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge utaanza siku ya Jumanne, tarehe 29 Agosti, 2023 na utatanguliwa na vikao vya Kamati kumi na sita (16) za Kudumu za Bunge.

Kamati tano (5) zitatangulia kuanza vikao, ambapo nne kati ya hizo zitaanza vikao tarehe 07 Agosti, 2023, na
Kamati moja (Bajeti) itaanza tarehe 10 Agosti, 2023.

Kamati zingine kumi na moja (11) zitaanza vikao tarehe 14 Agosti, 2023. Kamati zitakazotangulia kuanza vikao ni hizi zifuatazo;
(i) Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC);
(ii) Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa
(LAAC);
(iii) Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma
(PIC);
(iv) Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo; na
(v) Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.

2.0 SHUGHULI ZA KAMATI WAKATI WA VIKAO

Shughuli zilizopangwa kutekelezwa na Kamati za Bunge katika kipindi hicho zinajumuisha maandalizi ya shughuli za Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge na shughuli nyingine za Ufuatiliaji na Usimamizi wa Shughuli za Serikali kama ifuatavyo;

(a) Uchambuzi wa Miswada ya Sheria. Shughuli hii itatekelezwa na Kamati mbili za Bunge; Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria na Kamati ya Bajeti. Shughuli hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 136(14) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023;

(b) Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge. Shughuli hii itatekelezwa na Kamati ya Sheria Ndogo kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari, 2023;

(c) Kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za utendaji. Shughuli hii itatekelezwa na Kamati Kumi na Moja za Kisekta kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (c) na (d) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari, 2023;

(d) Kuchambua Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2022 ili kushughulikia maeneo yenye matumizi mabaya ya fedha za umma.

Shughuli hii itatekelezwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa mujibu wa Kifungu cha 13, Kifungu cha 14 na Kifungu cha 15 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023; na

(e) Kupokea na kuchambua Taarifa za Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ili kubaini iwapo uwekezaji huo una ufanisi na kuwa umezingatia taratibu na miongozo mujarabu ya biashara.

Shughuli hii itatakelezwa na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kwa mujibu wa Kifungu cha 11 (1) na (2) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023.






















































Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news