OUT wakoleza tabasamu kwa wanafunzi wa kike

DAR ES SALAAM-Katika kipindi cha Baragumu Live cha Channel Ten Julai 31, 2023 majira ya saa moja na dakika ishirini (1:20) asubuhi, Dkt. Mohamed Maguo aliwasilisha mada kuhusu Special Foundation Program ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kama ifuatavyo;
Mosi: Lengo la programu hii au mradi huu ni nini? Lengo la mradi huu ni kuwafikia wahitimu wa kike wa kidato cha Sita wa Masomo ya Sayansi ambao wana sifa za ufaulu wa angalau E na S katika masomo mawili ya tahasusi zao.

Tahasusi hizo ni PCM, PCB, CBG, PGM, CBA na EGM. Pia, wahitimu wa Diploma wenye ufaulu wa GPA 2.9-2.0 na wenye NTA level 5/Professional Technician level II Certificate.

Wahitimu wenye sifa hizi watajiunga na foundation program ambapo watapata mafunzo ya kina na hakika kwa njia ya ana kwa ana pamoja na mafunzo kwa vitendo kwa kipindi cha miezi mitatu.

Pili: Wahitimu hawa ni wale ambao wanaotokea katika familia zenye changamoto mbalimbali kama vile wanaotoka maeneo ya pembezoni, familia maskini, wenye ulemavu na yatima nk.

Hawa watapewa kipaumbele. Sababu hizi zimepelekea wanafunzi hawa kutopata sifa za moja kwa moja kujiunga na elimu ya juu.

Aidha, mradi huu unalenga kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike katika elimu ya juu kwenye fani za sayansi, teknologia, uhandisi, afya nk


Tatu: Ufadhili wa masomo hayo ya Special Foundation utatolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ufadhili huo utahusisha ada na gharama zingine za mwanafunzi na chuo. Kwa ufupi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itagharamia kila kitu kwa asilimia 100.


Nne: Jinsi ya kutuma maombi, waombaji wanaweza kufika kwenye vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambavyo vipo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar; Unguja na Pemba. Pia, wanaweza kuzipata fomu hizo katika tovuti ya www.out.ac.tz na kuzijaza kisha kuzituma kupitia barua pepe ofpheet@out.ac.tz

Muombaji anaweza kutuma maombi yake akiwa popote pale Tanzania bure bila gharama yoyote. Maombi yatapokelewa mpaka tarehe 5/8/2023 ambayo itakuwa ndiyo siku ya mwisho ya kupokea maombi. Baada ya tarehe hiyo kazi ya kupitia fomu za waombaji itaanza kufanywa na kamati maalumu ya kitaifa inayoshughulikia ufadhili huu.


Tano: Wahitimu watakaomaliza programu hii watapata sifa ya kujiunga na shahada ya kwanza katika vyuo mbalimbali hapa nchini. Wahitimu hao watapata fursa ya kuomba mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wakiwa katika masomo yao ya shahada.


Sita: Mradi huu ni wa miaka mitano (5) na utahusisha ufadhili wa wanafunzi Elfu Moja (1000) ambapo kila mwaka watafadhiliwa wanafunzi Mia Mbili (200). Huu ni ufadhili kwa wahitimu wa kike kwa asilimia mia moja kama ilivyoelezwa hapo juu.


Saba: Wanafunzi hawa wa Special Foundation Program watafundishwa kwa kutumia mfumo wa ana kwa ana na hivyo Saa za masomo kwa mujibu wa mtaala zitakamilika katika kipindi cha miezi mitatu. Sambamba na mafunzo ya ana kwa ana pia mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji Kieletroniki (Moodle), mihadhara mubashara kwa ZOOM, What's App vimbwete, Telegram vimbwete na ZOOM vimbwete itatumika.


Nane: Wanafunzi ambao hawatafaulu au kutimiza vigezo wataendelea na masomo kwa njia za kawaida na kufanya mitihani ya marudio (Supplementary). Watakaoshindwa mitihani ya majaribio, ufadhili huu utasitishwa.

Tisa: Taarifa kuhusiana na ufadhili huu wa masomo zinapatikana katika ofisi za Halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar.

Taarifa pia zinapatikana kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na tovuti ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. "Ewe muombaji mwenye sifa tuma maombi yako mapema kabla ya tarehe ya mwisho ambayo ni 05/08/2023.


Kumi: Shukurani za dhati ni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye aliyetoa fedha za serikali kwa ajili ya mradi huu.

Hii ni kutokana na kuona umuhimu wa kuwaendeleza watoto wa kike katika masomo ya sayansi na teknolojia kwa maendeleo ya Taifa letu.

Vilevile, shukurani za dhati ni kwa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ambao ndiyo wasimamizi Wakuu wa mradi huu na ndiyo walioongoza katika kuweka Mipango yote ya kuwezesha kufanyika kwa mradi huu.

Sambamba na Wizara ni wadau wa Elimu ya Juu wote ikiwa ni pamoja na TCU, NACTVET na Vyuo Vikuu vya Tanzania.

Wadau wote hawa kwa pamoja wamewezesha kukamilika kwa maandalizi yote na kukubali programu hii maalumu ifundishwe na wahitimu wake watajiunga masomo ya shahada za kwanza kwenye vyuo hivyo baada ya kuhitimu.

WENU
Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri Mwandamizi
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news