Rais Dkt.Samia aishukuru Simba SC

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewapongeza wana Simba kwa kumwalika kushiriki katika siku yao (Simba Day).

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa pongezi hizo leo Agosti 6, 2023 saa chache baada ya kushiriki katika tukio hilo kubwa ambalo limefanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

"Ahsanteni wana Simba kwa kunialika kushiriki nanyi katika siku yenu muhimu hii leo. Hongereni kwa siku nzuri. Pongezi kwenu kwa kuendelea kutangaza utalii wa nchi yetu kwa kufikisha kibegi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

"Michezo inatuleta pamoja, inatupa burudani, na kudumisha amani na utulivu, lakini pia inachagiza katika kukuza uchumi wa nchi yetu.

"Tumekuwa na mwamko na mafanikio makubwa katika michezo miaka ya karibuni. Mbali na Klabu ya Yanga kutinga fainali za Kombe la Shirikisho; Tembo Warriors, Kilimanjaro Queens na Serengeti Girls wametuwakilisha vyema kimataifa. Ahadi yangu ya hamasa ya kununua kila goli katika mashindano ya kimataifa itaendelea.

"Mbali na Serikali kuendelea kuwekeza katika michezo, natoa wito pia kwa sekta binafsi kufanya hivyo. Nchi yetu ina mazingira mazuri ya kufanya biashara, na michezo ni moja ya eneo muhimu kiuwekezaji,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news