Rais Widodo ziarani nchini leo

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko Widodo anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa nchini kuanzia leo Agosti 21,2023 hadi Agosti 22, 2023.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 21, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt.Stergomena Tax (Mb) wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea kuhusiana na ziara hiyo.

Mheshimiwa Dkt.Tax amebainisha kuwa, ziara hiyo ni matokeo ya kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine.

"Ziara ya Mheshimiwa Widodo itakuwa ni ziara ya pili kwa kiongozi wa taifa hilo kutembelea nchini. Ziara ya kwanza ilifanywa Mheshimiwa Soeharto, Rais wa Pili wa Indonesia tarehe 5 Disemba 1991, miaka 32 iliyopita.

"Mheshimiwa Rais Widodo atawasili tarehe 21 Agosti,2023 na atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 22 Agosti, 2023, Ikulu Dar es Salaam,"amefafanua Waziri Dkt.Tax.

Aidha, amesema baada ya mapokezi, viongozi hao watakuwa na mazungumzo ya faragha, na baadaye mazungumzo rasmi.

"Baada ya mazungumzo rasmi, kutakuwa na hafla ya utiaji saini Hati za Makubaliano ya ushirikiano kwenye ekta mbalimbali kama afya, nishati, madini, uchumi wa buluu, ushirikiano wa kimataifa, uhamaji na biashara na kuzungumza na waandishi wa habari."

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Tax amesema,baadaye Mheshimiwa Rais Widodo atashiriki dhifa ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na Mheshimiwa Rais kwa heshima yake.

"Siku hiyo hiyo pia, Mheshimiwa Rais Widodo atatembelea Ofisi ya Ubalozi wa Indonesia uliopo hapa nchini kabla ya kuhitimisha ziara yake na kuondoka nchini."

Waziri Dkt.Tax chimbuko la uhusiano kati ya Tanzania na Indonesia ni Mkutano wa Bandung uliofanyika mwaka 1955 ambapo nchi nyingi za Afrika na Asia zilikuwa katika utawala wa kikoloni kwa kipindi hicho.

"Kupitia mkutano huo nchi hizo zilikubaliana kuimarisha ushirikiano ili kujikomboa kutoka katika utawala wa kikoloni, na ulikuwa ndiyo msingi wa kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi zisizofungamana na Upande Wowote (Non- Aligned Movement-NAM).

"Hivyo, Tanzania na Indonesia zina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria. Uhusiano huo uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Indonesia Mheshimiwa Soekarno."

Mheshimiwa Dkt.Tax amesema, uhusiano wa kidiplomasia ulianza mwaka 1964, ambapo Indonesia ilifungua Ubalozi wake nchini mwaka 1964 na kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kufungua Ubalozi wake nchini miaka michache baada ya uhuru. Aidha,Tanzania ilifungua Ubalozi wake nchini Indonesia mwaka 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news