Msajili wa Hazina aweka wazi mikakati

NA GODFREY NNKO

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema, ofisi hiyo inafanya mageuzi katika muundo na utaratibu wa kusimamia mashirika na taasisi za umma ambapo pamoja na mambo mengine imependekeza kuanza utaratibu wa kuajiri na kufukuza watendaji wakuu wa mashirika hayo.

"Sasa haya tunayotaka kuyafanya tumeyakopa kutoka baadhi ya nchi,China tulikuwa tunaangalia wanafanyaje,TR (Ofisi ya Msajili wa Hazina) wanafanyaje, wao wanaita SASAC (State-owned Assets Supervision and Administration Commission of the State Council (SASAC)."

Mchechu ameyabainisha hayo Agosti 20,2023 mbele ya Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma katika siku ya pili ya kikao kazi kinachoendelea jijini Arusha.

SASAC ambayo ilianzishwa mwaka 2003 na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ina jukumu la kusimamia biashara zinazomilikiwa na Serikali (SOEs), ikijumuisha kuteua watendaji wakuu na kuidhinisha muunganisho wowote au mauzo ya hisa au mali, pamoja na kuandaa sheria zinazohusiana na SOEs.


"Ni bodi imara, inasimamia makampuni yao makubwa, lakini nimeangalia sheria yao, wajibu wao hautofautiani kabisa na wajibu wetu sisi tulionao.

"Wanatakiwa wasimamie mali zinazomilikiwa na Serikali, hicho ndicho tunachotakiwa kukifanya Tanzania, wanasimamia uwekezaji unaofanywa na mashirika na kudhibiti utendaji wake, ndivyo Sheria ya TR inavyotuambia tufanye, kuandaa sera zinazodhibiti mapato na matumizi ya mashirika, ndiyo TR tunvyofanya Tanzania.

"Kusimamia mageuzi na mifumo ya utendaji katika mashirika ikiwa ni pamoja na kukuza mfumo wa kisasa wa uanzishwaji wa biasha, ndiyo TR tunavyofanya Tanzania, kuendesha marekebisho ya kimkakati ya kimpangilio na muundo wa uchumi, ndiyo TR tunatakiwa tufanye Tanzania.

"Kuteua na kuwaondoa watendaji wakuu wa mashirika,labda hili sisi ndiyo hatulifanyi.Tunapendekeza sasa ili tuweze kufanya vizuri.

"Kwa hiyo ukiangalia yote haya SASAC wanayafanya, tunayo sisi TR, lakini ni kwamba hatujacheza mpira kwa viwango.

"Ni kama ambavyo timu zetu za Simba na Yanga wana sheria zile zile 17 za FIFA na zile timu zetu za daraja la kwanza sijui premium league, lakini mpira wetu ndiyo huo huo.

"Tumeenda kuangalia Kuwait nayo ukiangalia, Singapore ni kitu hicho hico, kwa hiyo tunajaribu kubuni mifumo ambayo itaenda na itasomana pia na wenzetu, ndiyo maana tunaangalia wenzetu wamefanya nini na mafanikio yao yamekuwaje, lakini kuna mafanikio makubwa.

"Kuna mafanikio ya kuwezesha kukuwa kwa kasi kwa sekta zao, kukuza miradi mikubwa, kuvutia wawekezaji na mengine mengi."

Amesema kuwa, azimio hilo ni moja ya mapendekezo ya kuboresha ofisi hiyo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema ameyapitisha.

Katika hatua nyingine, Msajili wa Hazina amebainisha kuwa, kuna wimbi la watumishi ambao wanakimbilia kuomba uhamisho kutoka katika taasisi zao kwenya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Sambamba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Udhibiti Nishati na Maji (EWURA).

Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo wa siku tatu ambao unaendelea jijini Arusha kuwa,maombi kwenda taasisi hizo ni mengi kwani,watu wanataka kwenda huko kwa kuwa mapato ni mazuri.

Wakati huo huo, Msajili wa Hazina amesema, anakusudia kukutana na Bodi na Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).

Amesema, lengo la kukutana huko ni ili wakubaliane namna ya mashirika hayo makubwa kuongeza mchango wa gawio katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mchechu amesema, TANESCO na NHC wamekuwa wakichangia zaidi ya shilingi bilioni mbili kila moja, ingawa kiasi hicho ni kidogo.

“Tunataka wachangie zaidi, hamuwezi kutupa shilingi bilioni mbili,” amesema akifafanua kuwa Hazina inahitaji taasisi hizo kuchangia zaidi ili sehemu ya mapato hayo yakawe mtaji kwa taasisi zingine za umma zenye uhitaji nchini.

Aidha,katika taarifa za Ofisi ya Msajili wa Hazina idadi ya taasisi zilizochangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali kupitia gawio zimepungua kutoka 236 mwaka 2019 hadi taasisi 108 mwaka 2023 huku mapato yakiongezeka kutoka shilingi bilioni 695.8 hadi shilingi bilioni 777.1.

Pia, michango ya taasisi binafsi ambazo Serikali ina hisa chache imeongezeka kutoka shilingi bilioni 58 mwaka 2019 hadi shilingi bilioni 231.2 mwaka 2023 huku ongezeko hilo likitokana na taasisi 15 ambazo ni nusu ya taasisi 30 zilizochangia mwaka 2019 nchini.

Katika hatua nyingine, Msajili wa Hazina amebainisha kuwa, wanatarajia kufanya mageuzi makubwa zaidi ambayo yataongeza ufanisi kwa baadhi ya mashirika kwa kuijumuisha Serikali, wawekezaji pamoja na wananchi.

"Tunataka haya mashirika, mengine tuyarudishe kwa umma, sasa tunayarudishaje kwa umma, maana yake tunakwenda kuyalist (kuyaorodhesha katika Soko la Hisa) na major focus kubwa ni kwenda kuyalist.

"Actually tuna model nzuri,tuangalie trend ya NMB au ya kupitia NMB ya kwanza ambayo tulienda tukatafuta strategic investor, halafu baadae tukaenda tukai-list, fikiri kuhusiana na combination ambayo tunayo leo.Tunayo Serikali, tunayo wawekezaji wa kimkatati, na tumewawezesha wananchi kumiliki, huenda hii model ni nzuri."

Wakati huo huo, katika wasilisho lake, Msajili wa Hazina amezungumzia kuhusu uhuru wa mashirika ikiwemo kuajiri ingawa uhuru huo amesema una mipaka yake.

"Kuainisha aina bora ya utendaji wa taasisi kwa kubainisha uhuru wa kujiendesha, ambapo ili tumelianza kwa sababu tulishapewa maagizo, ambacho tunakwenda kukifanya ni kuchambua zaidi, lakini haitakuwa kila taasisi, taasisi nyingi ni zile ambazo sasa zipo tayari na zimetengeneza utawala bora ndani na zinaweza kujiendesha, zina mikakati yake mizuri na zinaeleweka."

Kwa nini ofisi hii?

Ofisi ya Msajili wa Hazina ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya Umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya Sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Ofisi inayojitegemea kimuundo.

Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) Ofisi ilikabidhiwa majukumu ya Shirika hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news