Saudi Arabia yatoa tamko walioinajisi Qur'ani Tukufu

RIYADH-Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia,Prince Faisal bin Farhan amezitaka nchi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuungana katika juhudi za kuchukua hatua za kivitendo na madhubuti za kukabiliana na maandamano yanayohusisha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia,Prince Faisal bin Farhan. (File/SPA).

Wito huo ameutoa Julai 31, 2023 katika Mkutano Maalum wa OIC ambao ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya kushughulikia matukio ya mara kwa mara ambapo nakala za Qur'an zimenajisiwa nchini Sweden na Denmark hivi karibuni.

Prince Faisal alisema kuwa,jumuiya hiyo ilikuwa na jukumu la kutetea maadili ya uvumilivu na amani, kulinda na kueneza sura halisi ya Uislamu, na kukataa na kupambana na kutovumiliana na misimamo mikali.

Alisisitiza kwamba, juhudi za mataifa ya OIC zilisababisha Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio mnamo Julai 12 ambalo lililaani na kukataa vikali utetezi wowote na udhihirisho wa chuki za kidini, ikiwa ni pamoja na vitendo vya hadharani na vilivyotawaliwa kabla vya kuinajisi Qur'ani Tukufu.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje alisema kuwa, uhuru wa kujieleza unapaswa kuwa tunu ya kimaadili inayoeneza heshima na kuishi pamoja miongoni mwa watu na sio chombo cha kueneza chuki na migongano kati ya tamaduni.

Alisisitiza haja ya kueneza maadili ya uvumilivu na kiasi, na kukataa aina zote za mazoea zinazozalisha chuki, vurugu na itikadi kali.

Mwanamfalme Faisal alirejelea angalizo kali la Ufalme dhidi ya matukio ya kudhalilisha Qur’an, akisisitiza kwamba vitendo hivi vya uchochezi haviwezi kukubalika kwa uhalali wowote.

Katibu Mkuu wa OIC, Hissein Brahim Taha alitoa wito kwa Sweden na Denmark kuzuia kuchafuliwa kwa Qur'an na kuelezea kusikitishwa kwake huku kukiwa hakuna hatua zilizochukuliwa katika suala hilo hadi sasa.

"Inasikitisha kwamba mamlaka zinazohusika zinazodai uhuru wa kujieleza zinaendelea kutoa nafasi za kurudia vitendo hivi kinyume na sheria za kimataifa, na hii inasababisha kukosekana kwa heshima kwa dini,"Taha alisema katika hotuba yake wakati wa mkutano huo.

Msururu wa hivi karibuni wa matuko ya kuinajisi Qur'an yaliyofanywa na wanaharakati wachache wanaopinga Uislamu nchini Denmark na Sweden yameibua maandamano ya hasira katika nchi za Kiislamu.

Mapema siku ya Jumatatu, uchomaji moto zaidi wa Qur'ani uliendelea katika nchi za Sweden na Denmark huku serikali za nchi hizo mbili za Nordic zikisema kwamba zinachunguza njia za kisheria za kuwekea vikwazo vitendo hivyo kwa nia ya kupunguza mvutano unaoongezeka kati ya nchi hizo na nchi za OIC.

Siku ya Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Lars Lokke Rasmussen alisema kuwa, serikali itajaribu kuifanya iwe kinyume cha sheria kuinajisi Qur'ani au vitabu vingine vitakatifu vya kidini mbele ya balozi za kigeni katika nchi hiyo ya Nordic.

Pia,alisema katika mahojiano na shirika la utangazaji la umma la Denmark la DR kwamba, kuchomwa kwa maandiko matakatifu huwa kunachochea kuleta migawanyiko katika ulimwengu ambao unahitaji umoja na mshikamano.(AN/DIRAMAKINI)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news