Sekta ya Kilimo inahitaji nguvu ya pamoja-Rweyendela

DAR ES SALAAM-Imebainishwa kuwa, Sekta ya Kilimo inahitaji nguvu ya pamoja kutoka sekta na idara mbalimbali nchini ili iweze kuwa na matokeo bora kwa ustawi bora wa wakulima, jamii na Taifa kwa ujumla.

Meneja Mkazi wa AGRA Tanzania,Vianey Rweyendela ameyabainisha hayo Agosti 24, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi cha pamoja kati ya taasisi hiyo na wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Hayo yanabainishwa ikiwa zimesalia siku chache kabla ya Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF 2023) kufanyika jijini Dar es Salaam.

Jukwaa hilo ambalo linatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania litafanyika Septemba 5 hadi 8, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini humo.

"Ukifika sokoni kununua gramu moja utaona haiwezekani kwa sababu umezoea kuzalisha magunia matatu kwa hekari ambayo ni shilingi 300,000.

"Lakini yule aliyezalisha magunia 20 atakuwa na milioni sita, kwa hiyo suala la uchumi ni suala linaloguza uzalishaji, ndiyo maana suala la mbegu tutalisisitiza sana."

Rweyendela ameendelea kufafanua kuwa, "masuala ya kisera ni muhimu na kilimo ni suala la sekta mtambuka, unapoongelea kilimo kuna Wizara ya Viwanda, mazingira ya biashara.

"Hapo hapo kuna suala la uchukuzi kwa sababu mahindi utayatoa mfano Sumbawanga kuyapeleka Mtwara, kama huna miundombinu huwezi,kuna Wizara ya Afya masuala ya sumu kuvu, lishe kwa hiyo kilimo ni suala mtambuka," amefafanua Meneja Mkaazi huyo wa AGRA Tanzania.

"Sasa tunawezaje kuzileta sekta zote pamoja kuaongelea kilimo kama suala mtambuka, kuongelea mifumo ya chakula...kwa sababu unaweza kuwa na mahindi ukayatoa shambani unaongelea mtu anakula ugali, kuna watu wengi sana pale katikati.

"Suala la ushirikishwaji tayari Serikali toka ngazi ya Rais mmemsikia kila siku anaongelea suala la kina mama na vijana kwenye kilimo.

"Mahali ambapo kumekuwa na ushirikishwaji wa kundi jingine na ndio uchumi wa Tanzania unavyokuwa, uchumi unaweza kuwa unakuwa, lakini kwa asilimia ngapi.

"Kila siku mnasikia watu wanalalamika uchumi unakuwa mbona hatuoni, na kilimo kimeajiri zaidi ya asilimia 65 ukitaka kuwa na uchumi ambao unakuwa na unawafikia wananchi wengi lazima twende kwenye kilimo chenyewe.

"Tuko kwenye mipango ya AGRF kuna mtu ambaye hajui AGRF ni nini jamani? Bahati nzuri kila mtu anafahamu ya AGRF ya kwanza ilifanyika Ghana 2011 ikiwa ni mkakati uliokuwa wa Kofi Annan (Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa).

"Ninakumbuka mimi mwenyewe nilishiriki. Tulikuwa na Mheshimiwa Pinda (Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Pinda) tukafanya fujo nyingi wee..ee AGRF ikaletwa Arusha Tanzania mwaka 2012.

"Mwaka jana tulikwenda Kigali nchini Rwanda tukafanya fujo nyingine tukiwa na Makamu wa Rais pakawepo na mchakato mkubwa hatimaye Tanzania sasa ina-host AGRF msije mkafikiria hii AGRF imekuja Tanzania kwa bahati mbaya,hapana.

"Kuna watu wamepambana, kulikuwepo na proposal, interviews,viongozi wamekuwa interviewed kueleza watafanya nini, kwa hiyo nchi imetoa ahadi ya ku-host AGRF sasa."

Katika hatua nyingine, Meneja Mkaazi wa AGRA Tanzania,Vianey Rweyendela amebainisha kuwa, pakiwepo na sera himilivu ambazo haziyumbishwi na kauli za viongozi kadri wanavyobadilika zitawasaidia wakulima kupiga hatua.

"Zile sera za kubadilikabadilika, akija huyu anasema hivi, akija huyu pia anasema hivi, tunataka kuwa na sera imara ambazo haziyumbiswi na kauli za viongozi na kuwahakikishia wafanyabiashara mtafanya biashara katika mazingira haya.

"Mmemsikia Waziri wa Kilimo, Bashe (Mheshimiwa Hussein Bashe) kila siku anasema mkulima anauza anavyotaka, mara nyingi anakuwa anasema vile kwa hiyo tunataka hata akija Waziri mwingine naye aseme hivyo hivyo."

Pia amebainisha kuwa, ili kuongeza uzalishaji vivyo hivyo zinahitajika bidhaa bora za kilimo zinazotokana na uzalishaji huo.

"Tunahitaji kuona ubora katika uzalishaji, ni jambo la msingi sana, pia kujenga mifumo unapokuwa unasema kesho utafanya kitu fulani lazima kifanyike.

"Tunajenga mifumo, wanafanya wanakuwa na mifumo ambayo inakuwa endelevu na kuwasaidia wakulima kuuza mazao yao."

Aidha, Meneja Mkaazi huyo akizungumzia kuhusu masoko amesema kuwa,yanapaswa kuwa jumuishi na shirikishi ili yule mkulima anayezalisha mazao yake aweze kunufaika na kazi yake.

"Kuhusu masoko ni muhimu,pia kilimo endelevu, sote tunafahamu kwamba kilimo endelevu climate change inasumbua.

"Climate change ina vitu vingi sana vya kwenda navyo, kuna artificial intelligence, afya ya udongo suala la upatikanji wa mikopo na kuangalia tunamfanyaje mkulima kuwa na essintials, matumizi bora ya pembejeo.

"Wataalamu wanatuambia kwamba ukianza na mbegu bora, kuna watu wanatuambia mbegu za asili...mbegu za asili tunashindwa kuelewa.

"Kuna mbegu za asili za mahindi au mfano mpunga, mihogo mazao ya viazi ulaya haviwezi kuwa ni asili kwa sababu vyenyewe si asili sasa uasili wake unatoka wapi?.

"Kwa hiyo mtu ana-recycle halafu unamwambia ni asili na tunaelewa kabisa uki-recycle mbegu kuna kitu kinaitwa genetic gene kitapotea?.

"Yaani mbegu ukiendelea kui-recycle uzalishaji wake unapotea,kuna mtu anasema mbegu ya asili, sasa mahindi yamekuwaje asili Tanzania? Toka lini mahindi yamekuwa asili?"

"Mahindi yamekuja mwaka 1910 hapa zao jipya kabisa halafu unasema zao asili, kwa hiyo tunaongelea kwamba lazima pawepo na msisitizo wa utumiaji wa mbegu bora ambazo zimethibitishwa nchini na kama taifa wameweka mamlaka inayothibitisha mbegu.

"Na kila mbegu inayouzwa ina nembo, wewe ukinunua mbegu ambayo haijathibitishwa tayari unazuia ushindani wa soko, kwa sababu uzalishaji wako utakuwa wa chini na hivyo waandishi na wahariri mlielewe mnapo wasilisha taarifa zenu kwa wananchi waelewe utofauti wa mbegu bora na hizo mbegu wanazorudia rudia.

"Hawa wote wanawaambia mbegu ya asili, mbegu ya asili umerudia mbegu yako ambayo imepoteza genetic gain maana yake uzalishaji wake unakuwa chini ushindani wako pia kwenye soko unakuwa chini,"amefafanua Meneja Mkazi huyo wa AGRA Tanzania.

Katika hatua nyingine, Meneja Mkaazi huyo amefafanua kuwa, AGRA imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za kilimo na kuhakikisha sekta ya kilimo inaleta tija kwa wakulima, jamii na Taifa.

Pia amesema, kumekuwa na mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na sekta hii ya kilimo ambayo imepelekea nchi kuwa na utoshelevu wa chakula.

Meneja Mkazi wa AGRA Tanzania,Vianey Rweyendela amesema, mafanikio hayo yametokana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mageuzi katika sekta hiyo nchini.

“Serikali ya Awamu ya Sita imevunja rekodi kwenye sekta ya kilimo, kumekuwa na mabadiliko makubwa sana,kwani sasa wakulima wanalima kwa faida."

Rweyendela amesema, katika mkutano wa AGRF wamejipanga kuja na ripoti ya Hali ya Kilimo Afrika na mambo mengine mbalimbali yanayohusiana na sekta hiyo.

Sekta ya Kilimo barani Afrika ni miongoni mwa sekta muhimu ambazo zinategemewa na mataifa mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha utoshelevu wa chakula,malighafi kwa ajili ya makampuni mengi ya utengenezaji wa bidhaa za kilimo,na utoaji wa mapato kwa ajili ya kuendeshea miradi ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news