Simba SC yaitafuna Power Dynamos FC

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Simba ya jijini Dar es Salaam imeonesha makali yao kwa mabingwa wa Zambia, Klabu ya Power Dynamos baada ya kuichapa 2-0.

Ushindi huo wameupata katika siku yao ya Simba Day ambayo imesherehekewa katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Waliochana nyavu katika mtanange huo wa kirafiki ni Leandre Willy Essomba Onana dakika ya tano na Fabrice Luamba Ngoma dakika ya 75 ya mchezo huo.

Katika mchezo huo ambao mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wana Simba kwa kumwalika kushiriki katika siku yao (Simba Day).

"Ahsanteni wana Simba kwa kunialika kushiriki nanyi katika siku yenu muhimu hii leo. Hongereni kwa siku nzuri. Pongezi kwenu kwa kuendelea kutangaza utalii wa nchi yetu kwa kufikisha kibegi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

"Michezo inatuleta pamoja, inatupa burudani, na kudumisha amani na utulivu, lakini pia inachagiza katika kukuza uchumi wa nchi yetu.

"Tumekuwa na mwamko na mafanikio makubwa katika michezo miaka ya karibuni. Mbali na Klabu ya Yanga kutinga fainali za Kombe la Shirikisho; Tembo Warriors, Kilimanjaro Queens na Serengeti Girls wametuwakilisha vyema kimataifa. Ahadi yangu ya hamasa ya kununua kila goli katika mashindano ya kimataifa itaendelea.

"Mbali na Serikali kuendelea kuwekeza katika michezo, natoa wito pia kwa sekta binafsi kufanya hivyo. Nchi yetu ina mazingira mazuri ya kufanya biashara, na michezo ni moja ya eneo muhimu kiuwekezaji,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Ushindi huo ambao ulikuja baada ya shamrashamra, shangwe na utambulisho wa wachezaji ambapo Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ alikiweka wazi kikosi mapema.

Kikosi ambacho mwalimu huyo alikiweka wazi kwenye mchezo huu ambao Wanasimba wameiona timu yao kwa mara ya kwanza kuelekea msimu mpya wa mashindano 2023/24 waliopangwa walikuwa ni;

Ally Salim (1), Shomari Kapombe (12), Mohamed Hussein (15), Che Fondoh Malone (20), Henock Inonga (29), Sadio Kanoute (8), Willy Essomba Onana (7), Mzamiru Yassin (19), Kibu Denis (38), Said Ntibazonkiza (39), Clatous Chama (17).

Wachezaji wa Akiba:

Ahmed Feruzi (31), Israel Patrick (5), David Kameta (3), Kennedy Juma (26), Hussein Kazi (16), Fabrice Ngoma (6), Aubin Kramo (24), Abdallah Hamis (13), Jean Baleke (4), Moses Phiri (25), John Bocco (22), Peter Banda (11). Hussein Abel (30).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news