Simba SC yawanyoa Mtibwa Sugar

MOROGORO-Klabu ya Simba imeanza vema msimu wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya kujikusanyia alama tatu zikisindikizwa na mabao manne.

Ni katika mchezo wao wa kwanza Agosti 17, 2023 wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 4-2 katika mtanange uliopigwa Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.

Jean Baleke aliwapatia bao la kwanza dakika ya tano akimalizia mpira wa krosi uliopigwa kwa mguu wa kushoto na Kibu Denis kutoka upande wa kulia.

Aidha,Essomba Onana aliwapatia bao la pili dakika ya tisa kwa shuti la mguu wa kushoto akiwa ndani ya 18 kufuatia shuti la Baleke kuokolewa na mlinda mlango wa Mtibwa, Mohamed Makaka.

Kwa upande wao, Mtibwa Sugar FC walipata bao la kwanza dakika ya 20 kupitia Matheo Anthony kwa shuti kali ndani ya 18 akimalizia pasi ya Juma Liuzio.

Dakika mbili baadae Matheo aliisawazishia Mtibwa baada ya kupokea pasi ndefu na kuwazidi ujanja walinzi wa Simba SC akitokea upande wa kushoto.

Kiungo Fabrice Ngoma aliwapatia bao la tatu kwa kichwa dakika ya 44 kufuatia mpira mrefu wa krosi uliopigwa na Shomari Kapombe ambao ulimkuta Sadio Kanoute na baadae Baleke kabla ya kutua kwa mfungaji.

Clatous Chama aliwapatia bao la nne dakika ya 80 kwa shuti kali la mguu wa kushoto baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Luis Miquissone.

Tujikumbushe

Msimu wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambao ulianza Agosti 15, 2023 tulishuhudia timu ya Geita Gold FC ikiibuka washindi.

Ni kupitia bao pekee la Elias Maguri dakika ya tano ambalo lilitosha kuipa Geita Gold ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Ihefu SC katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ndani ya dimba la Highland Estate, Mbarali mkoani Mbeya.

Mbali na hayo,bao la Martin Kigi dakika ya 43 liliipa mwanzo mbaya Namungo FC nyumbani baada ya kuchapwa 1-0 na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ndani ya Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Vile vile,Dodoma Jiji FC waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ndani ya dimba la Jamhuri jijini Dodoma.

Wenyeji hao walipambana kufa na kupona, kwani walilazimika kutoka nyuma baada ya Coastal Union kutangulia na bao la dakika ya 46 Hijja Ugando, kabla ya wenyeji hao kuzinduka kwa mabao ya kipa Justin Ndikumana aliyejifunga dakika ya 54 na Meshack Abraham dakika ya 60.

Agosti 16, 2023 ikiwa ni mwendelezo wa michuano ya ligi hiyo yenye hadhi ya kipekee nchini, Mashujaa FC waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Wenyeji hao walipata ushindi ho katika mchezo wa baada ya kutembeza kandanda safi ndani ya dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.Mabao ya Mashujaa FC yalifungwa na Adam Adam dakika ya 15 na Othman Dunia dakika ya 73.

Katika hatua nyingine,Azam FC walianza vema Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kitayosce ya Tabora.

Ni kupitia mtanage uliopigwa ndani ya Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamazi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Azam FC yalifungwa na kiungo Feisal Salum Abdallah matatu dakika za tatu, tisa na 13 huku lingine likifungwa na Prince Dube Mpumelelo dakika ya tano.

Hii ilikuwa moja ya mechi za aibu baada ya kuishia dakika ya 18 kutokana na Kitayosce FC kubaki na wachezaji watano uwanjani baada ya wawili kati ya saba walioanza kuumia, hivyo kwa mujibu wa kanuni refa akamaliza mtanage huo.

Kitayosce ililazimika kuanza na wachezaji saba tu baada ya wengine wote kutokuwa na leseni za kuwaruhusu kucheza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news