Wadhamiria kutokomeza uhalifu

IRINGA-Viongozi wa kata na mitaa ya mjini Iringa wameshauri mambo manane ambayo kama yatatekelezwa yatasaidia kwa kiwango kikubwa kulinda na kupunguza uhalifu katika maeneo mbalimbali nchini.

Ushauri huo wameutoa katika kikao na Jeshi la polisi Mkoa wa Iringa kuhusu umuhimu na ufanisi wa Polisi Jamii, kilichoongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Urlich Matei kutoka Kamisheni ya Polisi Jamii Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dodoma.

Demitirio Matandula wa Mtaa wa Mlandege alitaja jambo la kwanza kuwa ni kuanzisha utaratibu utakaowalazimisha watu wanaohama mtaa mmoja kwenda mwingine kuwa na barua ya utambumbulisho kutoka kwa mwenyekiti wa mtaa anaohama kwenda mtaa anaohamia.

Pia, alilitaka jeshi hilo kuanzisha klabu za kupambana na uhalifu katika ngazi mbalimbali zikiwemo taasisi za elimu kama shule za msingi na sekondari ili zisaidie kuendesha mijadala itakayosaidia kuibua taarifa mbalimbali za uhalifu katika maeneo yao ili zifanyiwe kazi.

Mbali na utaratibu wa sasa unaotaka kila kata kuwa na askari kata mmoja, Suleimani Hamduni alishauri idadi ya askari iongezwe hususani katika kata zenye idadi kubwa ya watu ili kurahisisha polisi jamii kukabiliana kwa haraka na uhalifu.

“Na katika kuongeza uadilifu kwa jeshi letu, nashauri utaratibu wa zamani wa kuwapata vijana wanaotaka kujiungana jeshi hilo urudishwe,” alisema.

Alisema, utaratibu wa zamani ulikuwa unawataka vijana wanaoipenda kazi hiyo kuomba wakati wakimaliza shule za sekondari au vyuo tofauti na sasa ambapo vijana hao uomba kujiunga na jeshi hilo tu kwasababu wamekosa fursa katika maeneo mengine ya fani walizosomea.

Naye Edward Kilovela alishauri askari kata kupewa nyumba bora pamoja na motisha ya mafuta kwa wale wanaotumia vyombo vya vya usafiri wakiwa kazini kwasababu ya jeshi hilo kutokuwa na vyombo vya kukidhi mahitaji yake yote.

Kwa upande wake Abraham Mbilinyi wa Isakalilo alishauri nguvu za wananchi zitumike kufanikisha ujenzi wa vituo vya Polisi katika kila kata ili kurahisha upatikanaji na utoaji wa huduma za kipolisi karibu zaidi na wananchi.

Naye Galus Lugenge diwani wa kata ya Mwangata alisema jeshi la Polisi lianzishe utaratibu wa kutoa mrejesho wa kesi za waharifu waliokamatwa na polisi jamii katika maeneo yao kama sehemuya kuwajengea imani wananchi wanaoshiriki kupambanana uhalifu.

“Kuna wahalifu wanakamatwa na wananchi huko mitaani na baada ya kufikishwa vituoni, wapo wanaoachiwa bila wananchi kupewa sababu za kuachiwa kwao na hivyo kuwavunja moyo katika mapambano hayo,” alisema.

Aidha watendaji na wenyeviti hao wa mitaa wameshauri jeshi la polisi kuwa na vyombo vyake vya usafiri vya kutosha, liendelee kuemisha na liwashirikishe viongozi wa dini kwa kupitia maandiko yao kukabiliana uhalifu.

Awali, SACP Matei alisema jeshi la polisi limeendelea kutengeneza mazingira rafiki na jamii katika swala la ulinzi na usalama likiamini uhalifu uanzia katika ngazi ya mtaa.

“Suala la ulinzi na usalama sio la jeshi la polisi bali ni jukumu la kila mtu na ni muhimu wananchi kuhamasika katika imani za kiroho ili wamjue Mungu na waweze kuwa na mwenendo mwema katika jamii."

Kwa idadi yake alisema jeshi la Polisi halitoshelezi kufanya kazi ya ulinzi na usalama pekee yake, hivyo ni muhimu kwa watendaji wa ngazi zote katika kata kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ili vishiriki kutokomeza uhalifu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Allan Bukumbi aliwata watendaji na wenyeviti wao kwa kushirikiana na vikundi vyao katika maeneo yao kutoa kwa haraka taarifa za uhalifu na wahalifu ikiwa ni pamoja na kuanzisha madaftari ya wakazi yatakayosaidia kuwatambua wageni wanaohamia katika maeneo yao.

Kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia, ACP Bukumbi amewata viongozi hao katika mikutano yao kuzungumzia changamoto hiyo ili kujua chanzo chake na kujiwekea mikakati ya kukabiliana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news