Wahudumieni wananchi ipasavyo-Waziri Mkuu

MTWARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma kuwahudumia wananchi ipadavyo ili dhamira na maono ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kutoa huduma bora na kwa wakati yatimie.

“Serikali haitaki mzaha, kama wewe ni muajiriwa wa Serikali wewe ni mtumishi wa wananchi hivyo ni lazima uwahudumie. Watendaji nendeni vijijini kwa wananchi na kusikiliza kero si vema wakasubiri hadi viongozi wa kitaifa wanavyofika katika maeneo yao ndio watoe kero zao.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo Agosti 13, 2023 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Majaliwa uliopo wilayani Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara.

Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa watendaji wa Serikali kuwahudumia wananchi na kwamba Serikali iko makini katika kusimamia jambo hilo.

Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Tandahimba akamilishe taarifa ya uchunguzi wa mradi ya Kituo cha Afya cha Mambamba ambapo Serikali ilitoa sh milioni 500 na bado ujenzi wake haujakamilika.

Pia Mheshimiwa Majaliwa amesema baada ya kukamilika kwa taarifa hiyo apewe taarifa ya hatua zilichukuliwa kwa wahusika.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa huduma ya dawa katika wilaya hiyo amesema Serikali inatoa shilingi milioni 77 kila mwezi, hivyo hatarajii wananchi wanaokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wanakosa dawa.“Hakikisheni mnaleta dawa kulingana na magonjwa yanayowasumbua wakazi wa Tandahimba.”

Pia, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikagua na kuzindua mradi wa maji wa kata ya Kitama wenye thamani ya shilingi milioni 797 na kutumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana kulinda vyanzo vya maji kwa sababu vikiharibika watakosa huduma hiyo muhimu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprica Mahundi amesema mbali na mradi huo pia Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji wa Makonde wenye thamani ya shilingi bilioni 84 ambao utanufaisha wakazi wa wilaya za Newala na Tandahimba, hivyo amewahakikishia wakazi upatikanaji wa maji ya uhakika na salama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news