Waziri Mkuu atoa maagizo kuhusu wezi wa pembejeo

MTWARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza watendaji wote watakaobainika kuiba pembejeo za kilimo wachukuliwe hatua za kisheria kwa sababu wanaihujumu Serikali.

Pia amemuagiza Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Tandahimba Deogratius Mbowe amuhoji Afisa Kilimo wa Kata ya Kitama, Sharaf Manjavila kwa tuhuma za kuchukua pembejeo za wakulima.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Agosti 13, 2023 wakati akiongea na wananchi baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Kitama wilayani Tandahimba, Mtwara.

Awali, baadhi ya wananchi walimuomba Waziri Mkuu aondoke na Afisa Kilimo huyo kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake ikiwemo kumtuhumu kuiba pembejeo za wakulima wa korosho.

Wakulima hao walidai kuwa walifanyiwa uhakiki na kupewa namba ila wanapokwenda kuchukua pembejeo wanaambiwa hawajasajiliwa na majina yao hayajarudi, hivyo hawapewi dawa.

“Mashamba tulihakiki na namba tulipewa, tukifuata dawa tunaambiwa jina halijarudi na ukipeleka malalamiko yako makao makuu unaambiwa ulishachukua dawa, tatizo letu ni bwana shamba hafai.”

Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali itahakikisha kwamba suala hilo linasimamiwa vizuri, hivyo waendelee kuiamini na kushirikiana nayo.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba kwa kushirikiana na Afisa Kilimo wilaya wasimamie suala la ugawaji wa pembejeo katika wilaya hiyo.
Awali, Mheshimiwa Majaliwa alikagua na kuona juhudi za uongezaji thamani wa zao la korosho katika kiwanda Organic Growth Limited (OGL) kilichopo wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.

Alisema kiwanda hicho kitakapo kamilika kitaongeza thamani ya zao hilo kwa kuwa wakulima watapata fursa ya kwenda kubangua korosho zao na kuuza ikiwa imeongezwa thamani.

Waziri Mkuu alimpongeza muwekezaji huyo mzawa kwa uamuzi wake huo kwa sababu ujenzi wa kiwanda hicho unakwenda kuwapa wakulima soko la uhakika wa korosho zao.

Naye, Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Aldina Fakiri alisema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kubangua tani 3,000 za korosho ikiwa ni sawa tani 720 za korosho zilizobanguliwa kwa mwaka.

Alisema kiwanda ambacho kipo katika hatua za majaribio ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 3.5 kinatarajiwa kutoa ajira 200 kati yake 50 ni za kudumu na 150 zitakuwa za muda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news