Wanajua utamu wa Ligi Kuu msimu huu

DAR ES SALAAM-Unaweza kusema, kazi imeanza, kwani Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara imezidi kuwa ya moto huku kila mmoja akitafuta namna ya kuchomoka kivyake ili kwenda kuonja utamu wa ligi hii yenye vionjo vyake.

Watani wa jadi wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa, wanabakia katika kilele cha ligi hiyo ambayo imejizola umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania.

Licha ya Simba SC kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, wana Jangwani nao wameonekana wamepania sana Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, baada ya kuwashushia kitu kizito KMC FC kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mabingwa hao watetezi, Yanga SC wameanza ligi hiyo kwa kuitandika KMC mabao 5-0 usiku wa Agosti 23, 2023 Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamazi ndani ya Halmashauri ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Dickson Job dakika ya 17, viungo Stephane Aziz Ki dakika ya 58, mshambuliaji Hafiz Konkoni dakika ya 69 na viungo Mudathir Yahya dakika ya 76 na Pacome Zouazoua dakika ya 80 ndiyo waliozamisha jahazi la wana Kinondoni hao.

Aidham, huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Yanga msimu huu, huku KMC wakicheza mechi ya pili baada ya sare ya 1-1 ugenini na Namungo FC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Kagera Sugar vs Ihefu Fc

Agosti 19, 2023 bao pekee la Mubarak Hamza dakika ya 79 liliwapa wenyeji, Ihefu SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Unaweza kukiri wazi kuwa, Kagera Sugar imeendeleza rekodi mbaya ya mwanzo wa msimu wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kufungwa bao hilo na Ihefu.

Kagera Sugar tayari imepoteza michezo miwili msimu huu dhidi ya Mashujaa na Ihefu idadi sawa na michezo miwili ya mwanzo msimu uliopita ilipofungwa na timu za Azam na Simba.

Moubarack Amza kupitia ushindi huo aliiifanya Ihefu kupata ushindi wa kwanza msimu huu baada ya kufungwa na Geita Gold mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Aidha, Ihefu FC walitembeza kipigo cha pili kwa Kagera Sugar baada ya kuchapwa 2-0 na Mashujaa FC mjini Kigoma.

Namungo FC vs KMC

Pia,Namungo FC ilicheza mechi ya pili nyumbani ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara bila ushindi baada ya kutoa sare ya kufungana bao 1-1 na KMC.

Wawili hao walikutana katika mtanange ambao ulipigwa katika dimba la Majaliwa lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

KMC walitangulia kwa bao la Rashid Chambo dakika ya 69, kabla ya mshambuliaji Fabrice Ngoye kuisawazishia Namungo FC kwa penalti dakika ya 80.

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza katika msimu mpya kwa KMC, wakati Namungo mechi yao ya kwanza walifungwa 1-0 na JKT Tanzania hapo hapo Majaliwa.

Simba vs Dodoma Jiji

Katika hatua nyingine, Agosti 20, 2023 Klabu ya Simba imepata ushindi wa pili mfululizo katika Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao 2-0 na kukwea kileleni mwa msimamo kwa mara ya kwanza msimu huu.

Dodoma iliyoanza Ligi vema msimu huu kwa kuifunga Coastal Union mabao 2-1 ilishindwa kutamba mbele ya ‘Mnyama’ kwa mabao yaliyofungwa na Jean Baleke kipindi cha kwanza na Moses Phiri kipindi cha pili.

Mabao hayo yanaifanya Simba iliyofunga mabao sita kuwa kinara kwa kufunga mabao msimu huu mpaka sasa.

Mtibwa Sugar vs Coatal Union

Nao, Mtibwa Sugar wamelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Coastal Unión ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Wawili hao walichuana katika dimba la Manungu Complex lililopo Turiani mkoani Morogoro.Coastal Union walitangulia kwa bao la Ibrahim Ajibu dakika ya 70, kabla ya Kassim Haruna ‘Tiote’ kuisawazishia Mtibwa Sugar dakika ya 84.

Bao la mpira wa adhabu lililofungwa na Ibrahim Ajibu kwa Coastal na bao la Kassim Haruna yalifanya timu hizo kutoshana nguvu na kuendelea kusubiri kwa michezo inayofuata kupata ushindi wa kwanza msimu huu.

Geita Gold vs Mashujaa

Wakati huo huo, Agosti 21, 2023 Geita Gold imeendelea kung’ara ikicheza ugenini baada ya kupata suluhu dhidi ya Mashujaa FC kwenye uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Geita imeanza vema Ligi Kuu ya NBC kwa kukusanya alama nne katika michezo miwili bila kuruhusu bao lolote tofauti na msimu uliopita waliporuhusu mabao manne katika michezo miwili ya mwanzo.

Mashujaa FC iliyopanda daraja msimu huu imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Kagera Sugar na suluhu hiyo inaifanya timu hiyo kufikisha alama nne na kukaa nafasi ya pili ya msimamo wa ligi nyuma ya Simba.

SFG vs Tanzania Prisons

Vile vile, Singida Fountain Gate wamelazimishwa sare ya bila kufungana na Tanzania Prisons katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Mtanange huo wa mwendelezo wa michuano ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kati ya Singida Big Stars na Tanzania Prisons ulichezwa uwanja wa Liti, Singida saa 10:00 alasiri Agosti 22, 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news