Waziri Mkuu:Serikali inaendelea kuboresha huduma za Afya

MTWARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii nchini zikiwemo za afya, hivyo amewataka wananchi waendelee kuipa ushirikiano.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Newala Matiko Stephen, wakati alipokagua na kuweka jiwe la msingi la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Mtwara Agosti 14, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ameyasema hayo Agosti 14, 2023 wakati akizungumza na wananchi baada kuweka jiwe la msingi Hospitali ya Wilaya ya Newala akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara. Amesema kuwa Serikali imedhamiria kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Newala asimamie ipasavyo upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa sababu Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia huduma hiyo.

Waziri Mkuu amesema Serikali kila mwezi inapeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa hivyo hatarajii wananchi wanaokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wanakosa dawa. Amewasisitiza wapeleke dawa kulingana na magonjwa yanayopatikana katika wilaya hiyo.

Awali, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt… Matiko George alisema Serikali imetoa shilingi bilioni 2.85 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo jengo la maabara, wagonjwa wa dharura, huduma ya mama na mtoto, mionzi, utawala, wodi za wanawake, wanaume na watoto.

Alisema faida za mradi huo ni pamoja na punguzia gharama kwa wananchi ambao walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika halmashauri za jirani za Newala Mji, Masasi na Hospitali ya Rufaa ya Ndanda.

“Hospitali hii itakuwa na uwezo wa kufanya huduma za upasuaji kwa akina mama watakaokuwa wanapata changamoto ya kujifungua kwa njia ya kawaida. Pia huduma za za afya za kinywa na macho nazo zitatolewa hospitalini hapa.”

Pia, Dkt. George amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaa tiba vya kisasa katika hospitali za wilaya pamoja na vituo vya afya jambo linalowaongezea ari ya kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha, kuimarisha na kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya nchini. Vifaa tiba vilivyoko katika jengo la kutolea huduma za dharura kwenye hospitali hii vinalingana na vile vinavyotumika katika hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news