Askari wanyamapori wajeruhiwa kwa mkuki Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato

ARUSHA-Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imethibitisha tukio la kujeruhiwa kwa askari wa Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato mkoani Geita.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 1,2023 na Catherine Mbena,Afisa Uhifadhi Mwandamizi Kitengo cha Mawasiliano-TANAPA.

"Mnamo tarehe 31.08.2023 majira ya saa tano asubuhi, Askari Sita na Afisa mmoja wa Jeshi la Uhifadhi -TANAPA wakitekeleza majukumu yao ya Ulinzi wa Rasilimali za Taifa katika Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato walibaini ujangili wa nyama na kufanikiwa kukamata majangili wawili kati ya watatu waliokuwa wakiwinda hifadhini.

"Aidha, katika jitihada za kuwakamata majangili hao askari CRIII Wilson Lucas Mwita alishambuliwa kwa mkuki na kupata jeraha la mkuki kiganjani, na askari mwenzake CRI Pele Malima Taraba akijeruhiwa kwa mkuki tumboni.

"Majeruhi wote wawili walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa matibabu ya haraka (Emergency Care) ambapo CRIII Wilson Lucas Mwita alipatiwa matibabu na kuruhusiwa wakati mwenzake CRI Pele Malima Taraba amefanyiwa upasuaji.

"Na anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari katika Hospitali ya Wilaya ya Chato. Watuhumiwa wawili, Jumba Pascal (38) na Amos Nyanda (18) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na jitihada za kumsaka mtuhumiwa aliyetoroka zinaendelea."

"TANAPA inatoa Onyo kali kwa majangili kuacha mara moja vitendo vya ujangili kwani kwa kufanya hivyo inawadhulumu watanzania wengine haki ya mapato yanayotokana na rasilimali hizi.

"Aidha, kwa wale wanaojeruhi na kuua askari wanaopambana usiku na mchana kutunza maliasili hizi tunawapa salamu:Tutawatafuta popote walipo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria,"amefafanua Catherine Mbena,Afisa Uhifadhi Mwandamizi Kitengo cha Mawasiliano-TANAPA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news