KUNYWA MAJI KWA AFYA YAKO

NA LWAGA MWAMBANDE

KWA mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC),maji si sehemu ya kundi la chakula, lakini maji yana umuhimu mkubwa sana kiafya katika kufanikisha kazi mbalimbali mwilini.

Pia viungo vingi vya mwili ili viweze kufanya kazi vizuri vinahitaji maji na zaidi ya asilimia 60 ya uzito wa mwili wa binadamu ni maji. Hivyo, maji husaidia mwili kufanya kazi mbalimbali na hii ni pamoja na uyeyushwaji wa chakula, usafirishaji wa virutubishi na ufyonzwaji wa virutubishi mwilini.

Aidha, maji husaidia katika kutengeneza maji maji yanayopatikana katika viungo vya mwili kama vile viwiko na magoti, hivyo kusaidia viungo hivyo viweze kufanya kazi vizuri.

Wakati huo huo, maji hurekebisha joto la mwili,husaidia kuzuia kuondoa uchafu na mabaki ya uchafu mwilini kwa njia ya jasho na mkojo,kupunguza uchovu wa mwili.

Sambamba na kuzuia uwezekano wa kupata baadhi ya magonjwa kama vile saratani ya tumbo na kibofu cha mkojo, na mawe kwenye figo hasa yanaponywewa kwa kiasi kinachotakiwa.

Kwa mtu mzima anashauriwa kunywa maji safi na salama kiasi cha lita moja na nusu kwa siku au glasi nane kwa siku. Pia mtu mzima anaweza kuongeza kiasi cha maji kwa kunywa kwa kutumia vitu vya majimaji kama vile supu, juisi ya matunda halisi na madafu.

Watoto walioanza kupewa chakula wenye umri kuanzia miezi sita na kuendelea wapewe maji kulingana na uhitaji wao na ni vyema wapewe maji baada ya kula na siyo kabla ya kula.

Lakini kwa watoto wachanga wenye umri chini ya miezi sita hairuhusiwi kiafya kupewa chakula na kinywaji chochote zaidi ya maziwa ya mama kwani maziwa ya mama yanavirutubishi na maji ya kutosha kulingana na mahitaji ya mtoto.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ukifanikiwa kunywa maji kikamilifu licha ya mwili wako kuwa salama, pia utakabiliana na changamoto za kupoteza maji mwilini. Endelea;


1. Kunywa maji afya yako, na tena amani yako,
Kutokunywa sumu kwako, hatari ya afya yako,
Hivyo wapewa mwaliko, kokote kule uliko,
Tengeneza mwili wako, kwa hayo maisha yako.

2. Kunywa maji afya yako, zaidi ya kiu yako,
Mmeng'enyo mlo wako, ni unywaji maji yako,
Lainisha choo chako, na madikodiko yako,
Tengeneza mwili wako, kwa hayo maisha yako.

3. Hiyo afya ngozi yako, ni unywaji maji wako,
Lainisha ngozi yako, furahia utu wako,
Na ukavu mwili wako, ni kutokunywa maji kwako,
Tengeneza mwili wako, kwa hayo maisha yako.

4. Kwa afya ya figo yako, neema kwa mwili wako,
Kunywa maji dawa yako, tena utulivu wako,
Ondoa hatari kwako, silete mateso kwako,
Tengeneza mwili wako, kwa hayo maisha yako.

5. Maji ni furaha yako, kunywa kwa kicheko chako,
Kunywa maji nguvu zako, na tena uhuru wako,
Ni kujisikia kwako, tena utulivu wako,
Tengeneza mwili wako, kwa hayo maisha yako.

6. Kucheki uzito wako, kunywa maji afya yako,
Uzito wala si wako, maji yakiwa ya kwako,
Utabaki na kicheko, kwa wepesi mwili wako,
Tengeneza mwili wako, kwa hayo maisha yako.

7. Mwili siyo soda zako, sukari siyo ya kwako,
Sitake kumbushwa huko, iwe ni kawaida yako, uyanywe saizi yako,
Si kutibu kiu yako, hiyo ndiyo afya yako,
Tengeneza mwili wako, kwa hayo maisha yako.

8. Uwaulize wenzako, wanokunywa maji huko,
Uchote faida huko, ujenge tabia yako,
Katika ratiba yako, maji yawe bora kwako,
Tengeneza mwili wako, kwa hayo maisha yako.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news