MOYO NI MAISHA YAKO, UTUNZE UTAKUTUNZA

NA LWAGA MWAMBANDE

SEPTEMBA 29, 2023 Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema takwimu za wizara hiyo kupitia MTUHA (DHIS -2) zinaonesha, kumekuwa na ongezeko la asilimia 9.4 kwa magonjwa ya Moyo na Shinikizo la Juu la Damu pekee kutoka wagonjwa milioni 2.5 mwaka 2017 hadi wagonjwa milioni 3.4 mwaka 2022.
Picha na awarenessdays.

Ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.

Waziri Ummy amesema taarifa za ufuatiliaji wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka mwaka 1980 hadi mwaka 2020 inaonesha ongezeko la magonjwa ya Shinikizo la Juu la Damu na Kisukari katika jamii kutoka asilimia 1 hadi 9 kwa wagonjwa wa kisukari na kutoka asilimia 5 hadi 26 kwa wagonjwa wa Shinikizo la juu la Damu.

Vile vile amesema, magonjwa haya mawili ndiyo chanzo kikuu cha magonjwa ya Moyo, Figo pamoja na ugonjwa wa Kiharusi hivyo ongezeko hili ni tishio kwa ustawi wa afya ya jamii yetu.

Amesema, magonjwa ya Moyo na ugonjwa wa Kiharusi yanaweza kuzuilika kwa mtu mmoja mmoja na jamii yetu kwa kuweza kuchukuwa hatua za haraka.

“Kwa mujibu wa maelezo ya wataalam sababu zinazopelekea kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya kiharusi ni pamoja na kutozingatia ulaji unaofaa ambapo kwa nchi yetu inaonesha asilimia tatu tu ya watu wazima wanatumia kiasi cha wastani wa kutosha cha matunda na mbogamboga."

Waziri Ummy amesema idadi ya watu wazima wanaofanya mazoezi imeongezeka ukilinganisha na vijana huku akiwasihi kutenga muda zaidi wa kufanya mazoezi

Pia, amesema kupunguza matumizi yaliyokithiri ya chumvi, sukari na mafuta ya kupikia kwa kuzingatia ushauri wa muhimu unaotolewa na madaktari kwa kufanya hivi kutaweza kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo tatizo la moyo.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kuipongeza Serikali kwa jitihada mbalimbali inazofanya ya kuwekeza katika sekta ya afya iweze kutoa huduma bora kwa wananchi anasema,moyo ni maisha yako, hivyo yafaa uweze kuutunza na utakutunza. Endelea;

1. Moyo wako utumie, kuulinda moyo wako,
Na wala usitumie, kuumiza moyo wako,
Ni elimu iingie, afya kwa maisha yako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

2. Moyo ukutumikie, katika maisha yako,
Damu ukusukumie, ufanye shughuli zako,
Wala usiulalie, maumivu yake yako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

3. Lishe bora jipatie, usidhuru moyo wako,
Vingine usitumie, kwa afya ya moyo wako,
Tena usizidishie, sababu ya raha zako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

4. Wasemayo usikie, kuutunza moyo wako,
Ukitaka usalie, wewe na uhai wako,
Wala usipuuzie, hiyo ni hasara kwako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

5. Ulipo usibakie, fanya mazoezi yako,
Tena vema jipangie, ufanye kwa afya yako,
Mazoezi upatie, uwe vema moyo wako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

6. Vingine usitumie, kutibu tamaa yako,
Hata ujizidishie, uukere moyo wako,
Kesho isije ulie, yakija maradhi kwako,
Moyo ni maisha yako, utunze, utakutunza.

7. Chumvi mbichi situmie, inadhuru afya yako,
Chakulani jipikie, kiasi saizi yako,
Mtu usimvizie, ufanye kwa afya yako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

8. Maji vema utumie, yafaa mwilini mwako,
Viungo viyatumie, uwe mwema mzunguko,
Moyo nguvu zisalie, utumike huko kwako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

9. Ni vema ufikirie, kuhusu maisha yako,
Vema moyo utumie, ufanyapo mambo yako,
Siyo mpaka uumie, hasara kwa moyo wako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

10. Vijavyo viachilie, visiwe moyoni mwako,
Kama watu waambie, yagusayo moyo wako,
Usifanye visalie, viumize moyo wako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

11. Kicheko na kisalie, ni afya ya moyo wako,
Huzuni isibakie, inatesa moyo wako,
Ili wewe usalie, tunza vema moyo wako,
Moyo ni maisha yako, utunze utakutunza.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news