Rhobi Samwelly ayapa neno mashirika yasiyo ya kiserikali Mara

NA FRESHA KINASA

MJUMBE wa baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO) Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Uwezo wa Mshirika Tanzania, Rhobi Samwelly ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Mara kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa 'Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto mkoani humo.

Rhobi ameyasema hayo Septemba 29, 2023 wakati akitoa salama za NaCoNGO katika uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Uwekezaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara uliopo Mjini Musoma.

Katika uzinduzi huo, viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Polisi pamoja na wadau kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali wamehudhuria uzinduzi huo.

Rhobi amesema, mashirika yasiyo ya kiserikali yakifanya kazi kwa ufanisi na weledi watoto ambao ndio tegemeo kwa taifa la baadaye watakuwa katika makuzi salama, maadili mema, na kuondokana na changamoto za kufanyiwa vitendo vya ukatili.

"Kuna watoto pia ambao tumekuwa tukiwapokea katika vituo vya Nyumba Salama wana umri mdogo sana ambao hukimbia ukeketaji, na vitendo vingine vya ukatili lazima tushiriki kuhakikisha watoto wanalimdwa dhidi ya aina yoyote ya ukatili,"amesema Rhobi.

Pia, ameyataka mashirika yanayotekeleza miradi mbalimbali mkoani Mara kuendelea kukemea mila na desturi zenye madhara ikiwemo vitendo vya ulawiti, ubakaji, na ukeketaji ambavyo watoto wamekuwa wakifanyiwa jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Wanawake na Makundi Maalumu ameishukuri Wizara ya TAMISEMI kuushusha mpango huo uweze kutekelezeka ngazi ya chini katika kuwafikia walengwa ambao ni Watoto wa miaka 0 hadi 8.

Miriam amesema, maeneo ya Mpango huo ni pamoja na lishe bora, afya Bora, malezi yenye mwitikio, Ulinzi na Usalama wa mtoto, fursa za ujifunzaji wa awali.

Amesema, mpango huo unalenga kuwa na matokeo ya wazazi, walezi familia na Jamii kuwa wamejengewa uwezo wa kutekeleza taratibu sahihi za malezi jumuishi pamoja na mazingira wezeshi yameboreshwa kuwezesha uratibu wenye ufanisi na utoaji huduma za malezi jumuishi.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara,Marco Maduhu akizungumza katika kikao hicho, amewaomba Viongozi wa dini Mkoani Mara kuwa sehemu ya kuimarisha maadili mema kwa kutoa mafundisho ya kiroho ambavyo yatawajenga waumini ili kuwa na kizazi salama katika kipindi hiki ambacho mmomonyoko wa maadili umekuwa tishio.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news