Ofisi ya Rais-Utumishi watakiwa kurejea na ubingwa SHIMIWI

DODOMA-Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Leila Mavika ameisisitiza timu ya Ofisi hiyo inayokwenda kushiriki kwenye michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu kuhakikisha inashindana ili kuibuka kidedea.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Leila Mavika akiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza na wanamichezo 46 wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo hao waliochaguliwa kushiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa.

Katika michezo hiyo ya kusisimua iliyopangwa kufanyika Mkoani Iringa, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora imepeleka wachezaji 46 ambao watashindana katika michezo ya mpira wa miguu, netiboli, baiskeli, pamoja na riadha.

Mwaka 2014, Ofisi hiyo ilishiriki katika michezo hiyo na kufanikiwa kunyakua ubingwa, ambapo tangu mwaka huo haikuweza kushiriki tena hadi mwaka huu.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,UTUMISHI, Bi. Leila Mavika akizungumza wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo 46 waliochaguliwa kushiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa.

Akizungumza wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo hao 46 waliochaguliwa kwa ajili ya kuipeperusha bendera ya Ofisi hiyo katika michezo ya mwaka huu, Bi. Mavika amewahimiza wawakilishi hao kuhakikisha wanakwenda kupambana kikamilifu ili kurejesha heshima ya Ofisi hiyo katika michezo hiyo.

“Kwanza kabisa napenda kuwapongeza kwa kuchaguliwa kuiwakilisha Ofisi katika michezo ya SHIMIWI ya mwaka huu, kwani Ofisi hii ina watumishi wengi lakini mmechaguliwa nyinyi, hivyo ni lazima mjue mmepewa heshima kubwa sana ya kutuwakilisha,” amesema.
Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Utawala kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Nyasinde Mukono akizungumza wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo 46 waliochaguliwa kushiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa.

Pamoja na kuwataka wakacheze kikamilifu na kurudi na ubingwa, Bi Mavika amewaasa watumishi hao kuonyesha nidhamu ya hali ya juu, ndani na nje ya uwanja.

“Lazima mkumbuke mnakwenda kuiwakilisha Ofisi yenye heshima ya juu sana katika Serikali yetu, hivyo mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa na wengine,” ameongeza.

Hata hivyo, amewatia moyo kwamba uongozi wa Ofisi hiyo utasimama bega kwa bega na wachezaji hao katika kipindi chote cha mashindano, na kuwataka wasisite kuwasiliana na uongozi wa Ofisi pale watakapokutana na changamoto yeyote.
Kwa upande wake, mwakilishi wa timu hiyo, Bw. Charles Shija, ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kuwaamini na kuwapatia huduma nzuri katika kipindi chote cha maandalizi.

“Tunajua Ofisi kwa sasa ina vipaumbele vingi na vya muhimu sana vya kutekeleza, lakini pamoja na hayo mmeona umuhimu wa kuturuhusu na kutuwezesha kushiriki katika mashindano ya mwaka huu, tunaahidi hatutawaangusha,” amesisitiza Bw. Shija.

Aidha, amesema wachezaji wote wana afya nzuri na wamepata muda mzuri wa kufanya mazoezi chini ya makocha hodari hivyo wana uhakika wa ushindi na kurudi na ubingwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news