Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo Sekta ya Utalii

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezitaka taasisi zote zinazohusiana na usimamizi wa Sekta ya Utalii nchini, kuhakikisha wajasiriamali wa ndani wanapewa kipaumbale kunufaika na fursa zinazopatikana kwenye sekta ya utalii hususani masoko ya bidhaa wanazozalisha.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Septemba 25,2023 kwenye hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi alipofungua Tamasha la Fahari ya Zanzibar.

Sambamba na maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Wakala wa Uwezeshaji wa Nchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA).

Alisema, hali hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi zinazoweza kuzalishwa Zanzibar na kuimarisha soko la ndani kwa wajasiriamali wake.

“Nazitaka taasisi zote zinazohusiana na usimamizi wa sekta ya utalii nchini, kuhakikisha wajasiriamali wa ndani wawe wanufaika wa kwanza kwa fursa zinazopatikana kwenye sekta ya utalii.
"Hali hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa uingizaji wa bidhaa tunazoweza kuzizalisha, kutoka nje ya nchi na kuimarisha soko la ndani kwa wajasiriamali wetu,”ameagiza Rais Dkt.Mwinyi.

Rais Dkt.Mwinyi alisema, juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi ni kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya Zanzibar kwa bidhaa wanazozizalisha, aliongeza uchumi wa Zanzibar una fursa nyingi za masoko kwa bidhaa za wajasiriamali wake kutokana na kuwepo kwa hoteli nyingi za utalii.
Dkt.Mwinyi aliwataka wajasiriamali na wafanyabiashara wa ndani kushirikiana na wadau wengine kuzalisha bidhaa zenye ubora kulingana na mahitaji na kunufaika na soko la utalilii liliopo.

Aliongeza, suala la kuwawezesha wananchi kiuchumi ni mtambuka kwa vile linahusisha wadau wengi na sekta mbalimbali zikiwemo Uchumi wa Buluu, Kilimo, Utalii, Biashara, taasisi za fedha, sekta binafsi na asasi zisizo za serikali za kitaifa na kimataifa.
Pia, Rais Dkt.Mwinyi alieleza taasisi zote hizo zina wajibu na dhima ya kutengeneza fursa za ajira kwa maendeleo ya Zanzibar yanayokwenda sambamba na sera ya taifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2022.

Alisema, dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha ongezeko la ajira kwa vijana na wanawake linaongezeka kwa kuendelea kutoa fursa nyingi na kuwawezesha kiuchumi kutokana na fursa za mikopo zilizopo.

“Serikali imejidhatiti kutimiza malengo ya ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 /2025 ya kuzalisha fursa za ajira laki tatu kwa kipindi cha miaka mitano.
"Ni dhahiri kasi iliyopo idadi hii haiwezi kusalishwa na ajira kutoka serikalini pekee bila shaka fursa nyingi za ajira zitatokana na kuwawesha wananchi kujiajiri ambapo wajibu wa Serikali ni kuandaa mazingira wezeshi kwa wananchi wake ili kujikwamua,”alieleza Rais Dkt.Mwinyi.

Alisema, Serikali inaendelea na hatua ya kuimarisha na kuinua maeneo ya biashara ikiwemo ujenzi wa masoko na maeneo muhumu ya kufanyia biashara kwenye maeneo ya vituo vya mabasi, lengo ni kuwapatia wafanyabiashara hao wateja wengi wa bidhaa zao kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Alisema, tamasha hilo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha na kuwaweka pamoja wadau wote pamoja na wajasiriamali mbalimbali kwa kubadilishana uzoefu kwenye tasnia hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga alieleza lengo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuendelea kutoa mikopo isiyo na riba kwa wananchi wake na kuwawezesha wajiajiri kupitia mikopo inayowapatia na kuyafikia malengo yao kiuchumi.

Alisema, wizara ilijipangia kuwakopesha wajasiriamali 12,000 kwa mwaka na sasa imefikia idadi ya 19,000 na kuongeza kuwa kiasi cha shilingi bilioni 20.2 zimekopeshwa kwa wananchi na kueleza mahitaji yameongezeka zaidi kutokana na maombi ya wananchi wengi yamefikia shilingi bilioni 80.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi, Juma Burhan Muhamed alisema taasisi hiyo imeingia makubalianao na taasisi mbalimbali wezeshi kwa wananchi zikiwemo, Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF),

Zanzibar Maisha Bora Foundation, TanTrade na taasisi nyingine ili kuwainua wajasiriamali wa ndani wakiwemo vijana, wanawake na wakulima wa mwani kwa kuendelea kuwatafutia soko la bidhaa wanazozizalisha.
Pia alieleza taasisi hiyo inaongeza uelewa kwa jamii kuthamini na kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ambapo wajasiriamali 19,373 walikopeshwa kiasi cha shilingi bilioni 20.2 kwa Unguja na Pemba.

Wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi Zanzibar ni taasisi iliyoundwa mwezi Machi, mwaka 2022 ikipewa jukumu la kutekeleza na kuratibu, shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news