Rais Dkt.Samia atema nyongo

DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa falsafa zake za maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na ujenzi mpya amezichukua kama msingi unaomuongoza katika kuongoza nchi ili isonge mbele kama Taifa kwa pamoja.

Amesema hayo Septemba 11, 2023 jijini Dar es salaam wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama Vya Siasa unaoshirikisha Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa kwa lengo la Kutathmini Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Kujadili Hali ya Siasa nchini.

Mhe. Rais Samia amesema kuwa, tayari Serikali imeshaanza kutelekeleza mapendekezo ya kikosi kazi ikiwemo kuruhusu kufanyika mikutano ya hadhara ambapo kwa sasa mikutano hiyo inafanyika sehemu mbalimbali nchini.

“Hatukutoa fursa ya mikutano ya hadhara ili watu kuvunja sheria, tumieni fursa hii kujenga sera zenu kwa wananchi na si vinginevyo.

"Hakuna aliye juu ya sheria, atakaye fanya kosa atachukuliwa hatua za kisheria, kila mtu adumishe amani, umoja na mshikamano wa kitaifa,”ameeleza Rais Dkt.Samia.

Ameongeza kuwa, kuna uhuru wa kutoa maoni, lakini una mipaka yake kisheria na kibinadamu na kuwa marekebisho ya Katiba yameanza kufanyiwa kazi, si mali ya vyama vya siasa bali ni mali ya Watanzania wote.

“Hatutakurupuka katika hili, tutaenda taratibu ili kuweka kila kitu sawa ikiwemo kutoa elimu kwa Watanzania ili kila mtu atoe maoni yake ya nini kibadilike, demokrasia sio matusi, demokrasia ni kutoa maoni, tusiitumie vibaya.

"Vyama vya Siasa nawakumbusha misingi yetu kufuatwa ambayo ni pamoja na kuheshimu maazimio yetu, kuheshimu sheria za Serikali, kuheshimiana,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.
 
Kuhusu Katiba

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia akizungumzia kuhusu mchakato wa Katiba mpya amesema, "Maoni yamekuja kila upande wale waliotaka peke yao Katiba.

"Kikosi cha siasa kikubwa Katiba, Zanzibar wote wamesema Katiba, na wote tulitoa kauli kwamba tumekubaliana na tunakwenda na marekebisho ya Katiba yetu.Tumekubaliana.

"Lakini jambo hili ni mchakato na kwa bahati nzuri, Katiba si mali ya wanasiasa, si mali ya vyama vya siasa ni ya watanzania awe ana chama , awe hana chama, awe ana dini awe hana.

"Awe mrefu awe mfupi , mnene mwembamba, mkubwa aumdogo, Katiba ni ya watanzania.Kwa hiyo, matengenezo yake yanahitaji tafakuri na kubwa sana hatuwezi kuchipuka tu pwaaa haya...

"Unachukua Katiba ya Warioba inasemaje, Katiba ya Kenya inasema, kifungu kinasemaje, hatuendi hivyo hii ni mali ya watanzania.Tunataka tukifanya marekebisho ituchukue muda kitabu chetu kiende...

"Lakini Katiba ni kitabu tunaweza kutengeneza kitabu kizuri, tukakipamba, tukakiweka, wangapi wanakielewa hicho kitabu? Yaliyomo humo ndani wangapi wanaelewa, Katiba tuliyonayo wanaielewa ?.

"Unakwendaje kumuuliza mtanzania nipe maoni yako wakati kitu haikijui, tunaanza na elimu ya watanzania wajue ni kitu gani, wajue kinasemaje, kina nini, lakini tunakwenda viongozi wa kisiasa huku tukidhani tuna haki ya kuburuza watu tunachokisema sisi watu wote waseme hivyo.

"Tnataka Katiba mpya, watu waseme , mtu ukimuuliza kifungu gani kinauzi hakuna!hajui ! au unataka nini kibadilike maana ndio tunataka mpya, tunataka mpya tu.

"Sasa mpya ilete nini ?Unajua ndio hivyo ndio maendeleo, nani kasema maendeleo yanaletwa na kitabu kilichotungwa kikawekwa pale? Kama kuheshimu vitabu tungeheshimu vya dini sio ndio vya kuheshimiwa?.

"Wangapi tunaviuka hatuvishemu, na huwezi kuheshimu kitabu mpaka ujue maana yake, hata cha dini huwezi kuheshimu Masihafu yako, Biblia yako kama hujui humo ndani kuna nini.

"Na ndio maana unaona kuna wengine wanachukua wanalala nayo, lakini matendo tofauti, hayaendani. Tunakwenda tunadhani tuna haki kuburuza watu tunachokisema sisi watu wote wakifuate tunageuza watu makasuku,"alifafanua Rais Dkt.Samia.

Naye, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuwa, Ofisi yake na Ofisi ya Makamu wa Rais Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mawaziri wa nchi wa ofisi hizo wameendelea kuratibu hatua kwa hatua hadi kuunda vikosi kazi.

Ni vikosi kazi ambavyo vimeendelea kufanya jukumu la kuratibu shughuli za kisisasa na hatimaye kuifikia hatua ya kuwa na mpango mkakati wa namna ya kwenda ili kuimraisha mwenendo wa vyama nchini.

“Mheshimiwa Rais tangu ulipoingia madarakani kwa dhamira yako na kwa nia njema yako uliona upo umuhimu wa vyama vyetu vya siasa kukaa meza moja kuzungumza lakini pia kupitia changamoto zinazozikabili kwa maslahi ya taifa.

"Leo hii tunakutana hapa ikiwa ni kikao cha kutathimini utekelezajii wa mapendekezo yaliyochakatwa na vikosi kazi vyetu na pia kujadili hali ya siasa nchini,”amebainisha Waziri Mkuu Majaliwa.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema kuwa, mikutano hiyo inasaidia kufungua fursa ambazo zimeminywa za wadau kukaa kwa pamoja na kueleza changamoto zinazowakabili.

“Mkutano huu umefurika kwa kuwa hatujawahi kuwa na mikutano ya aina hii ambayo inatusaidia kuondoa zile nyufa zinazokuwepo."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news