Tanzania yaibwaga UAE mwenyeji wa Mkutano wa Dunia wa Ufugaji Nyuki 2027

SANTIAGO-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshinda nafasi ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Dunia wa Ufugaji Nyuki (APIMONDIA) kwa mwaka 2027.

Uamuzi huo umefikiwa Septemba 8, 2023 jijini Santiago nchini Chile baada ya Mkutano wa Mwaka wa 48 wa Dunia wa Ufugaji Nyuki uliofanyika jijini humo kuanzia Septemba 4 hadi 8,2023

Rais wa APIMONDIA, Jeff Pettis amesema, usiku wa Septemba 8, 2023 kuwa,Tanzania imepewa nafasi hiyo kwa kukidhi vigezo vyote vya maandalizi ya mkutano huo, baada ya kuingia raundi ya mwisho na kupambana na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Katika mkutano huo wa Dunia wa Kongresi ya Wafugaji Nyuki Duniani unatarajiwa kuleta pamoja takribani watu 4,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu Maliasili na Utalii, Kamishna Bennedict Wakulyamba, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof.Dos Santos Silayo na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili, Dr. Deusdedit Bwoyo.

Kwa nini Tanzania?

Mbali na sababu nyingi ambazo zinaipa hadhi Tanzania kuwa wenyeji wa mkutano huo, pia ufugaji nyuki ni miongoni mwa sekta muhimu za kiuchumi nchini, yenye mchango mkubwa kwenye maisha ya watu wengi mijini na vijijini.

Aidha, sekta hii inakadiriwa kuajiri zaidi ya watu milioni mbili nchini kwenye mnyororo wake mzima wa thamani.

Mazao ya nyuki kama vile asali, nta, chavua, gundi ya nyuki,maziwa ya nyuki na sumu ya nyuki, yanatumika yakiwa kwenye hali tofauti pia kama malighafi ya viwanda vya chakula, urembo,dawa, nguo, ngozi, umeme na mishumaa.

Pia, ufugaji nyuki umedhihirisha kuchangia ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa kuongeza ubora wa mbegu na uhifadhi wa bioanuai kwa njia ya uchavushaji unaofanywa na nyuki. Kutokana na umuhimu kwenye uchavushaji, ufugaji nyuki umetambuliwa kama nyenzo ya uhifadhi.

Aidha, Tanzania ina hekta za misitu milioni 48.1 inayofaa kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki. Kwa sababu hiyo, sekta inakadiriwa kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali na tani 9,200 za nta kwa mwaka.

Licha ya uwezo uliopo, uzalishaji wa sasa ni tani 30,400 na 1,830 za asali na nta mtawalia kwa mwaka. Sekta inazalisha fedha za kigeni zipatazo Yuro milioni 7.96 kutokana na mauzo ya asali na Yuro milioni 1.59 kwa mauzo ya nta kwa mwaka.

Ili kufikia uzalishaji wa juu wa asali, serikali imeandaa mikakati mbalimbali ya kuwezesha maendeleo ya sekta ya ufugaji nyuki:

Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, Sheria ya Ufugaji Nyuki Na. 15 ya mwaka 2002, Kanuni za Ufugaji Nyuki za mwaka 2005, Mwongozo wa Udhibiti wa Ubora wa Mazao ya Nyuki wa mwaka 2007,

Viwango vya Udhibiti wa Ubora wa Asali na Nta vya mwaka 2006 (TZS: 2006) na Mpango Mkuu wa Taifa wa Utafiti wa Ufugaji Nyuki (2020-2030).

Sheria nyingine zinazosimamia sekta ya ufugaji nyuki ni pamoja na: Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002, Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009,

Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2004 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999.

Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998 inahimiza uanzish waji,usimamizi na umiliki wa Hifadhi za Nyuki na Manzuki.

Sheria ya Ufugaji Nyuki namba 15 ya mwaka 2002 inaelekeza taratibu za uanzishwaji wa Hifadhi za Nyuki. Pia, inahimiza kutengwa kwa maeneo ya kutosha ya misitu kwa lengo la kuendeleza na kusimamia makundi ya nyuki na kuongeza uwezo wa uzalishaji na matumizi ya mazao ya nyuki.

Sambamba na Sheria ya Ufugaji Nyuki,Sheria ya Ardhi ya Vijiji inatoa fursa kwa jamii kusimamia maliasili zao kwa kuwapa nguvu wananchi katika ngazi za vijiji kupitia mikutano mikuu ya vijiji, kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi ya kawaida au usimamizi wa maliasili.

Apimondia ni nini

Apimondia ni Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na Ufugaji Nyuki Duniani ambalo huleta pamoja wanasayansi, wataalamu na wafugaji nyuki kutoka duniani kote na mwaka wa 2023 Chile ilikuwa mwenyeji wa tukio hilo la kimataifa.

Mikutano yao mara nyingi mbali na kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo muhimu, imekuwa sehemu ya hamasa ya utalii na hata kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo muhimu.

Wakati wa Kongamano la Apimondia ambalo liliambatana na ApiEXPO limewawezesha washiriki kujenga mtandao mpana wa marafiki na kupokea mawazo mapya zaidi ya sayansi na ufugaji nyuki.

Kupitia Kongamano la 48 la Apimondia kulikuwa na siku tatu ambazo ziliangazia ufugaji nyuki endelevu katika ulimwengu unaobadilika.

Washiriki walipata wasaa wa kujuzana kwa kina ufugaji nyuki endelevu kwa kutumia kanuni za ikolojia, ambapo matumizi ya nyuki yanaheshimu sheria za mazingira.

Pia, walijuzana kuwa, ufugaji nyuki unaoheshimu mazingira unaweza kuwa endelevu na wenye faida, hata kama mabadiliko ya hali ya hewa yanafanya ufugaji nyuki kuwa na changamoto zaidi.

Aidha, waliangazia kwa kina bidhaa zilizoongezwa thamani kutoka kwenye mzinga, ambapo asali na nta ni bidhaa kuu ambazo wafugaji nyuki hutegemea.

Hata hivyo, chavua, gundi ya nyuki,maziwa ya nyuki na sumu ya nyuki ilielezwa ni bidhaa za thamani kutoka katika mzinga ambazo wafugaji wa nyuki wakubwa na wadogo wanaweza kutumia ili kuongeza faida kutokana na ufugaji nyuki.

Zaidi ya hayo, bidhaa hizi ni rasilimali muhimu za chakula na matibabu ambazo huchangia katika sekta ya chakula na dawa kuhakikisha afya bora ya binadamu.

Washiriki walijifunza namna ambavyo bidhaa zinavyoogezwa thamani na jinsi ya kuziunganisha katika ufugaji wao wa nyuki.

Pia, waliangazia kuhusu matumizi ya ardhi, bioanuwai na ufugaji nyuki, hii ni kutokana na ukweli kwamba,ufugaji nyuki unategemea kuwa na malisho bora na hii inathiriwa sana na kubadilisha mifumo ya matumizi ya ardhi.

Hasa, kilimo kikubwa, ukuaji wa miji na mabadiliko ya hali ya hewa hufanya iwe vigumu kupata maeneo mazuri ya nyuki wanaosimamiwa na kuathiri uchavushaji.

Apimondia 2027

Uenyeji wa Tanzania katika mkutano huo, unatarajiwa kuwa na neema kwa wafugaji nyuki wa Tanzania ambapo washiriki wote watapata nafasi ya kuwatembelea kwenye maeneo yao ya ufugaji nyuki.

Tarehe zinazopendekezwa kwa Apimondia Congress hiyo ni Septemba 20 hadi 25, 2027 ikijumuisha, ziara za kiufundi (siku moja hadi mbili) zitakazopangwa kabla na baada ya kongamano.

Pia, ukumbi unaopendekezwa uko katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mlima Kilimanjaro (MKAICC), uliopo Kijenge Estate jijini Arusha, Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news