Umeme wa REA kuchochea ukuaji wa uchumi vijijini

LILIAN LUNDO NA VERONICA SIMBA

WANANCHI wa Kijiji cha Ntanga kilichopo Kata ya Murusagamba Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wamejipanga kutumia fursa ya ujio wa umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuchochea uchumi wa mtu mmoja mmoja na kijiji kupitia umeme huo.

Diwani wa Kata Murusagamba, Mhe. Sudi Mkubira amesema hayo wakati wa mahojiano maalum kuelekea uwashaji wa umeme kijijini hapo Septemba 29, 2023, ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko atawasha umeme kijijini hapo.

“Tangu umeme umeingia kijijini, tayari watu wameshanunua ‘fridge’, watu wameshaanza kutafuta mashine za umeme kwa ajili ya kusaga, hata mashine za kutoa ‘photocopy’ tumeanza kupata,” amesema Diwani huyo.

Ameendelea kusema kuwa, ujio wa umeme kijijini hapo unatarajiwa kuleta maendeleo makubwa pamoja na kufungua fursa mbalimbali kwa wakazi wa kijijini hapo, vilevile wameanza kupokea wageni mbalimbali kutoka vijiji vya karibu wakifuata fursa za umeme.

“Tumejipanga kutumia fursa zinazotokana na umeme. Umeme una faida kubwa, unaweza kuwasha mashine, unaweza kuchomelea vyuma, unaweza ukachaji simu, unaweza kufanya shughuli mbalimbali kwa umeme,” amesema mwanakijiji wa Ntanga, Shedrack Kachinde.

Ameendelea kusema kuwa, kupitia umeme huo wa REA amejipanga kutafuta mashine inayotumia umeme kwa ajili ya kufanya shughuli za kinyozi kijijini hapo.

Naye, Marry Erick amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha Kijiji cha Ntanga kupata umeme, amesema kuwa kabla ya kufika umeme iliwabidi kufunga maeneo yao ya biashara mapema, tofauti na sasa ambapo wanaweza kufungua biashara mpaka saa mbili za usiku na kuendelea bila kuhofia usalama wao, kutokana na uwepo wa umeme.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news