Walinzi hawa wanasakwa kwa kushirikiana na majambazi kupora Arusha

ARUSHA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limeamua kuchua hatua za haraka kufuatia walinzi wa Kampuni ya Mengwe kutajwa kuhusika katika tukio la ujambazi jijini humo.

Kutokana na hali hiyo, kwa sasa walinzi wote Mkoa wa Arusha watahakikiwa.Walinzi wawili wa kampuni hiyo wanasakwa kwa tuhuma za kuhusika na ujambazi, kwenye makazi ya Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Predators Safari Club LTD, Yusuph Khan eneo la Kiranyi Sakina mkoani Arusha. 

Walinzi wa kampuni hiyo pamoja na watuhumiwa wengine wanatuhumiwa kuiba shilingi 30 milioni na vidani vya dhahabu vyenye thamani ya shilingi 15 milioni, Septemba 10 na kukimbia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema, wameanza kuhakiki wafanyakazi wa kampuni za ulinzi kwa kuchukuwa alama za vidole na kupata taarifa zao ili kuzihifadhi.

"Tutapita kwenye hizi kampuni na kuchukuwa alama za vidole na taarifa za wafanyakazi, kwani watu wanakodisha hizi kampuni za ulinzi ili walindwe, lakini siyo kuibiwa," amesema Kamanda Masejo.

Amesema, kutokana na tukio hilo la wizi polisi bado wanaendelea na uchunguzi na tayari wakurugenzi wa Kampuni ya Mengwe wamehojiwa na wametakiwa pia kushirikiana na vyombo vya dola kuwakamata watuhumiwa.

"Tumewahoji tayari na wameendelea kutupa ushirikiano ili kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa," amesema.


Meneja wa Kampuni wa Mengwe Security, Juma Masuka amesema, wafanyakazi wawili wa kampuni hiyo, Moses Alfred Mabula (46) na Lazaro Richard Pyuza (37) wanasakwa kwa tuhuma za kushiriki katika ujambazi.

"Bado tunawatafuta hawa walinzi ambao walionekana kwenye kamera za CCTV wakiwa wanawafungulia geti majambazi, lakini pia walishiriki kupora kwa kuwaweka chini ya ulinzi Khan na familia yake na baadae kukimbia," amesema.

Amesema, walinzi hao waliokuwa ni wakazi wa eneo la Daraja Mbili wamekimbia tangu kufanya ujambazi huo, lakini watahakikisha wanakamatwa na akatoa wito wananchi watakaowaona kutoa taarifa polisi.

Kampuni ya Predators Safari imetangaza kutoa zawadi ya shilingi 2 milioni kwa ambao watafanikisha kukamatwa watuhumiwa hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news