Waziri Bashungwa awakingia kifua wakandarasi wa ndani

DODOMA-Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameagiza Wizara kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), kuhakikisha wanakuja na mikakati ya kuwawezesha Makandarasi Wazawa kushirki katika Utekelezaji wa miradi ya Sekta ya Ujenzi nchini ili kuleta tija kwa Makandarasi hao na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo Septemba 26, 2023 jijini Dodoma, wakati alipokutana na kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC).
Bashungwa ameagiza Wizara kukaa na kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kuandaa mikakati itakayosaidia makandarasi hao kutekeleza miradi mingi hasa ya kimkakati itakayoweza kuinua mitaji yao.

“Linapokuja suala la ‘Local content’ yaani fursa za kiuchumi kwa watanzania, Mheshimiwa Rais kiu yake ni kuona ushiriki wa makandarasi wazawa kwenye maendeleo ya Sekta ya Ujenzi unaongezeka”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa idadi ya Makandarasi waliosajiliwa na Bodi ni 14,550 ambapo kati ya hao 550 ni Makandarasi wa nje na 14,000 ni Makandarasi wazawa lakini katika utekelezaji wa miradi Makandarasi Wazawa wanapata asilimia 46 na Makandarasi wa nje wanapata asilimia 54.
Aidha, Bashungwa ameishukuru Serikali kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho aliyoayaagiza katika sheria ya manunuzi kwa miradi yenye gharama ya kutoka Bilioni 10 hadi 50 kupewa kipaumbele kutekelezwa na makandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo.

Kuhusu madeni kwa Makandarasi, Waziri Bashungwa amesema kuwa kupitia Wizara ya Fedha, Serikali imeshaweka utaratibu wa kulipa madeni hayo ambapo hivi sasa kila mwezi kuanzia mwezi wa nane kiasi cha Bilioni 70 kinatengwa ambapo Bilioni 50 zinalipa madeni ya makandarasi wa ndani na Bilioni 20 ni kwa ajili ya kulipa Makandarasi wa nje.

Bashungwa pia ameziagiza Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kuhakikisha zinabuni mikakati ya kutangaza mafanikio na kazi zao kwa umma ili kuleta tija katika Taasisi hizo na Taifa kwa ujumla.
Kadhalika, Bashungwa ameziagiza Taasisi hizo kusimamia wataalamu wao ili kuhakikisha wanatoa huduma sahihi na kwa wakati kwa umma na kuhakikisha wanachukua hatua kwa wale ambao watakiuka maadili ya kazi zao.
Akiwasilisha taarifa, Msajili wa Bodi ya CRB, Eng. Rhoben Nkori, amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Bodi imesajili jumla ya miradi 4,374 yenye thamani ya shilingi Trilioni 9.274 ambapo miradi ya shilingi trilioni 4.999 sawa na asilimia 53.9 ilitekelezwa na Makandarasi wa ndani na miradi ya shilingi Trilioni 4.275 sawa na asilimia 46.1 litekelezwa na makandarasi wageni.

Naye, Msajili wa Bodi ya ERB, Eng. Benard Kavishe, amesema kuwa Bodi inaratibu mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi wahitimu yenye lengo la kuwawezesha wahitimu hao kupata ujuzi na umahiri wa kutosha katika utendaji wa shughuli za kihandisi katika muda mfupi.

“Katika kusimamia na kuratibu moango huu wa mafunzo, Bodi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imeingiza katika mpango huu wanafunzi 873 na kwa mwaka wa fedha 2022/23 wanafunzi 2,113”, amefafanua Eng. Kavishe.
Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya AQRB, Arch. Edwin Nnunduma ameeleza kuwa Bodi imesajili jumla ya Wataalam 1,514 kati ya hao Wataalam Wazawa ni 1,481 na wageni ni 33. Kampuni za ushauri 455 kati ya hizo Kampuni za Wazawa ni 448 na za wageni 7. Kwa kipindi cha mwaka ujao wa fedha (2023/24) Bodi imepanga kusajili Wataalam 156 na Kampuni 30.

Sambamba na hayo, Mtendaji Mkuu wa NCC, Dkt. Matiko Nturi ameeleza kuwa kuwa Baraza hilo limefanikiwa kuandaa mapendekezo ya gharama za ujenzi wa barabara kwa kila mkoa wa Tanzania Bara na kuwasilisha katika kikao cha wadau wa ndani ya kupata maoni na ushauri wao.
Waziri Bashungwa anaendelea na ziara zake ya kutembelea na kuzungumza na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi ili kujionea maendeleo yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news