Iran yaionya Israel kuhusu Gaza, yasema Hezbollah wakiingia litakuwa tetemeko

BEIRUT-Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,Hossein Amirabdollahian siku ya Jumamosi Oktoba 14, 2023 alitoa wito kwa Israel kusitisha mashambulizi yake huko Gaza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amirabdollahian akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na mwenzake wa Lebanon, Abdallah Bouhabib, mjini Beirut, Lebanon.(Picha na Hussein Malla/AP).

Pia, alionya kwamba vita vinaweza kuenea katika maeneo mengine ya Mashariki ya Kati ikiwa Hezbollah itaingilia kati, na hiyo itaifanya Israel kupata kile ambacho alikiita tetemeko kubwa la ardhi.

Waziri Amirabdollahian aliwaambia waandishi wa habari mjini Beirut kwamba, kundi la Hezbollah la Lebanon limetilia maanani hali zote za vita na Israel inapaswa kusitisha mashambulizi yake huko Gaza haraka iwezekanavyo.

Israel inawachukulia Hezbollah kuwa tishio kubwa zaidi la mara moja, ikikadiria kuwa kundi hilo lina takribani roketi na makombora 150,000, yakiwemo makombora ya kuongozwa kwa mifumo ya kisasa zaidi na ambayo yanaweza kupiga popote nchini Israel.

Kundi hilo, ambalo lina maelfu ya wapiganaji walioshiriki katika mzozo wa miaka 12 wa Syria, pia lina aina tofauti za ndege za kijeshi.

Wapiganaji wa Hezbollah wamekuwa katika hali ya tahadhari katika mipaka ya Lebanon na Israel kufuatia shambulio la Jumamosi iliyopita lililofanywa na kundi la wapiganaji wa Palestina la Hamas ambalo lilisababisha vifo vya mamia ya raia na wanajeshi wa Israel.

Siku ya Jumamosi, jeshi la Israel lilisema shambulizi la ndege zisizo na rubani za Israel kwenye mpaka na Lebanon lilifanikiwa kudhibiti mifumo ya kijasusi iliyokuwa ikijaribu kupenyezwa ndani ya Israel.

Aidha, Siku ya Ijumaa, Hezbollah ilisema wapiganaji wake walirusha makombora kadhaa katika maeneo manne ya Israel kwenye mpaka.

Jumamosi alasiri, wapiganaji wa Hezbollah walirusha safu ya roketi na makombora katika maeneo ya Israel katika Mashamba ya Chebaa yenye mzozo. Wanajeshi wa Israel wameshambulia maeneo ya karibu Kusini mwa Lebanon.

Shirika la Habari la Serikali ya Lebanon liliripoti kuwa, mwanaume mmoja na mkewe waliuawa katika shambulio la makombora la Israel katika kijiji cha mpakani, huku Hezbollah ikisema kuwa mmoja wa wapiganaji wake pia aliuawa Jumamosi.

Amirabdollahian alijadiliana mjini Beirut siku ya Jumamosi kuhusu hali ya Gaza na eneo hilo na afisa mkuu wa Hamas aliye uhamishoni, Saleh Arouri, na kiongozi wa kundi la Palestina Islamic Jihad, Ziad Nakhaleh, kwa mujibu wa runinga ya Al-Manar ya Hezbollah.

Maafisa wa Hamas wamekuwa wakisema mara kwa mara kwamba shambulio la Jumamosi iliyopita katika eneo la Kusini mwa Israel na kuuwa zaidi ya raia 1,300 na wanajeshi lilikuwa ni kazi ya kundi la Palestina na Iran haina uhusiano wowote nayo. Maafisa wa Hamas hawakujibu wito wa Associated Press kuthibitisha na kutoa maelezo kuhusu mkutano huo.

Amirabdollahian aliondoka Beirut Jumamosi mchana kufuatia ziara iliyompeleka Iraq, Syria na Lebanon, ambako Tehran ina ushawishi mkubwa.

Mbali na hayo, Waziri Amirabdollahian alisema, alikutana Ijumaa na kiongozi wa Hezbollah, Sayyed Hassan Nasrallah, ambaye alimweleza kuhusu hali ya kundi hilo nchini Lebanon.

"Ninajua kuhusu mipango ya Hezbollah waliyojiwekea," Amirabdollahian alisema. "Hatua yoyote itakayochukuliwa na Hizbullah itasababisha tetemeko kubwa la ardhi katika kundi na ardhi ya Wazayuni.

"Nataka kuwaonya wahalifu wa kivita na wale wanaounga mkono chombo hiki kabla ya kuchelewa sana kukomesha uhalifu dhidi ya raia huko Gaza, kwa sababu inaweza kuwa kuchelewa sana, lakini saa chache zitajibu."

Awali Rais Joe Biden wa Marekani aliwaonya washirika au makundi mengine ya Mashariki ya Kati kutojiunga na mzozo huo na ametuma meli za kivita za Marekani katika eneo hilo na kuahidi kuiunga mkono kikamilifu Israel.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema atawasiliana na maafisa wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati kwa sababu,bado kuna fursa ya kumaliza vita.

Uwezekano wa kuwepo mapigano mapya nchini Lebanon unaleta kumbukumbu chungu za vita vikali vya mwezi mzima kati ya Hezbollah na Israel mwaka 2006 ambavyo vilimalizika kwa mkwamo na mvutano mkali kati ya pande hizo mbili. (ABC/Agencies)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news