Miradi ya NHC yaivutia Kamati ya Bajeti Zanzibar, watoa kongole

NA GODFREY NNKO

WAJUMBE wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuyawezesha mashirika ya nyumba nchini ili yatekeleze majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 6, 2023 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mheshimiwa Mwanaasha Khamis Juma baada ya kutembelea miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ikiwa ni sehemu ya ziara yao ya siku moja ya kulifahamu vyema shirika na kujifunza namna wanavyotekeleza miradi yao nchini.

Amesema, Serikali zote mbili kwa maana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa, mashirika hayo yanajengewa uwezo wa kutosha ili kuendelea kutekeleza miradi ya makazi bora kwa ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

"Tumejifunza mengi na tumeona tayari zaidi ya asilimia 95 ya nyumba katika majengo haya zimeshapata soko, tunawapongeza sana ikizingatiwa kuwa, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lina ushirikiano mzuri sana na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC)."

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.45 ya mwaka 1962. NHC baadae liliunganishwa na iliyokuwa Msajili wa Majumba kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 1990 ambayo ilirekebishwa mwaka 2005 ili kulifanya shirika lijiendeshe lenyewe kibiashara.

Malengo ya shirika kwa mujibu wa Mpango Mkakati wake (2015/16-2024/25) ni pamoja na kuwa msimamizi mahiri wa miliki, kuimarisha uwezo wa kiuendeshaji na udhibiti, kutumia kikamilifu rasilimali watu, kuwa kiongozi katika uendelezaji miliki, kuhuisha mikataba na mazingira ya kisheria na kujenga taswira ya shirika nchini.

"Lakini, huku Bara kuna mafanikio makubwa sana kupitia shirika hili, kwa hiyo nasi kama kamati ya bajeti tutaenda kushauriana kuona namna bora zaidi ya kuhakikisha tunafanya maboresho makubwa ili na wao (ZHC) wawe katika nafasi nzuri na Serikali au shirika liweze kupata mapato.

"Tunashukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya.

"Lakini pia na Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ili kuona maendeleo katika nchi yetu yanakuwa, lakini pia na Serikali iweze kuingiza mapato na kukusanya kodi."

Awali Sekta ya nyumba Zanzibar ilisimamiwa na kuendeshwa na Idara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira tangu mwaka 2000 hadi Agosti 2015.

Katika kipindi hicho, sekta hiyo ilikuwa ilionekana kuwa dhaifu na ilikuwa na mchango mdogo kwa Pato la Taifa. Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali ya Zanzibar iliamua kuanzisha Shirika la Nyumba (ZHC) mwezi Septemba 2015 ili kuimarisha sekta hiyo ili kukuza uchumi.

Licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali, Serikali zilizopitz ikiwemo ya Awamu ya Nane ambayo inaongozwa na Rais Dkt.Mwinyi imeendelea na juhudi kubwa za kuhakikisha shirika hilo linasimama imara ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya makazi nchini.

"Kwa hiyo sisi kama Kamati ya Bajeti ya Zanzibar kuna vitu vingi ambavyo tumejifunza NHC na tutaenda kuishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, namna gani inaweza kuliendesha Shirika la Nyumba Zanzibar kupitia yale ambayo tumejifunza mazuri katika eneo hili.

"Japo kuwa na kwetu mazuri yapo na wao wanajua kuna mazuri, kwa hiyo ni vizuri tukabadilishana, ya kule mazuri wanayachukua na sisi tunayachukua mazuri huku ili waweze kufanya vizuri zaidi na wananchi waneemeke.

"Kwetu kule tuna usemi Mheshimiwa Rais alisema Yajayo ni Neema Tupu, huku tuna usemi wa Mama Samia unasema Kazi Iendelee. Iendelee kwa maana kila kitu kifanyike kwa wakati ili maendeleo ya nchi na uchumi wetu ukue,"amebainisha Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bajeti.

Aidha, baada ya wajumbe hao kutembelea miradi ya NHC ukiwemo wa Morocco Square na mradi wa nyumba za makazi wa Samia Housing Scheme unaotekelezwa na shirika hilo katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam wameonesha kuridhishwa.

"Kupitia ziara hii, tumejifunza vitu vingi, miongoni mwa mambo ambayo tumejifunza ni namna ambavyo wenzetu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Tanzania Bara wanavyotekeleza miradi yao serious kabisa, tumetembelea Mradi wa Morocco Square na Mradi wa Samia Housing Scheme wa Kawe tumeona mengi.

"Lakini, pia tumejifunza kwamba wenzetu wapo serious sana katika kuwekeza,hapa wamewekeza Shirika la Nyumba la Taifa na hiki ni chanzo kikubwa cha mapato, na cha kufurahisha zaidi katika asilimia 95 ya majengo haya yameshapata soko."

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar, Mhe. Juma Makungu Juma ambaye aliambatana na wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar amesema, wamejifunza mambo mengi kupitia NHC na wanatarajia yatakuwa na manufaa katika sekta ya nyumba Zanzibar.

ZHC

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Mwanaisha Ali Said amesema, shirika hilo lipo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo nyumba za kuwapangisha watu wenye kipato cha chini Pemba na Unguja.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetenga ardhi ya akiba kwa ajili ya maendeleo, hivyo shirika litatumia fursa hiyo kujenga nyumba za kupangisha na kuuza kwa wananchi mbalimbali kwa ajili ya kuleta makazi bora nchini.
Mkurugenzi Mkuu huyo, amesema ZHC kwa sasa imeanza kujenga nyumba za kuuza katika eneo la Mombasa kwa Mchina.

"Kwa hiyo, katika kuendesha miradi yetu hii mipya, tumeona na tumejifunza mambo mengi, mfano mradi huu wa Samia Housing Scheme tumejifunza umuhimu wa kujenga kwenda juu zaidi,sisi kama kisiwa njia ya kupata nyumba nyingi ni kwenda juu zaidi.

"Na pia, kama shirika kuongeza kipato kwa muda mfupi, eneo ndogo, nyumba nyingi kwa hiyo tumekuja hapa kujifunza ili tuweze kufahamu wenzetu walivyoweza kufikia hatua hii, walivyojikwamua ili na sisi tuweze kusonga mbele."

Ujenzi wa nyumba za Mombasa kwa Mchina utagharimu shilingi bilioni 9.8 ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa shilingi bilioni 6.8 na Shirika la Nyumba Zanzibar ( ZHC) limetoa shilingi bilioni tatu.

NHC

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Hamad Abdallah amesema, ziara hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa ushirikiano ambao walisaini miezi kadhaa iliyopita jijini Dodoma.

Pia, Bw.Abdallah ametoa wito kwa taasisi nyingine kuiga ambayo wamefanya wao, kwani hatua hiyo inasaidia kila upande kujifunza mambo mapya kwa ajili ya maboresho makubwa na ustawi bora wa taasisi hizo za umma.

Mei, mwaka huu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar zikiwemo taasisi zake za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) zilisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya ardhi na nyumba nchini.

Kupitia makubaliano hayo maeneo ya utekelezaji katika ushirikiano huo ni kukusanya, kuchakata na kubadilishana taarifa za ardhi baharini.

Pia kubadilishana uzoefu kwenye maendeleo na matumizi ya mifumo ya habari na teknolojia kwa sekta ya ardhi pamoja na kuandaa na kutekeleza sera, sheria na miongozo mbalimbali ya sekta ya ardhi.

Maeneo mengine ni kushirikiana kitaalamu na kubadilishana uzoefu katika mfumo wa usimamizi na maendeleo ya sekta ya milki kuu inayojumuisha makaazi na nyumba, utafiti na maendeleo kwenye sekta ya ardhi.

Sambamba na utatuzi wa migogoro ya ardhi pamoja na ushirikiano na kubadilishana uzoefu katika usimamizi na maendeleo ya mji Mkongwe.

Pia, Bw.Abdallah licha ya kuendelea kuwapongeza wafanyakazi wote kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika miradi hiyo, ameendelea kuwapongeza wanawake kwa kuonesha ufanisi mkubwa katika kazi.

Amesema, Mradi wa Samia Housing Scheme unasimamiwa na mwanamke ambaye ni Mhandisi Grace na ameonesha juhudi kubwa tangu mradi huo unaanza hadi ulipofikia sasa.

Kutokana na juhudi hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mwanaasha Khamis Juma pia amewapongeza wanawake kwa kazi nzuri huku akisisitiza kuwa, imani ambayo taasisi na hata Serikali iliyonayo kwao ni kubwa, hivyo wachape kazi kwa bidii.

"Wanawake katika ujenzi huu wa miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mnaonesha bidii kubwa sana, tunaaminiwa na sisi imani hiyo tuzidi kuionesha kwa kufanya kazi kwa bidii.

"Na hata yale mambo ya kudokoadokoa tuna hofu, tunataka mambo yetu tunayoyasimamia yanyooke vizuri, hongereni sana kina-baba pia, mbele ya mafanikio ya kina-mama mjue nyuma kuna kina-baba na mbele ya mafanikio ya kina-baba basi nyuma kuna kina-mama, kwa hiyo hongereni sana kwa kazi nzuri."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news