NHC wapeleka tabasamu Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar

ZANZIBAR-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa vifaa tiba mbalimbali kwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja (MRH) jijini Zanzibar ikiwa ni utekelezaji wake Sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Vifaa tiba hivyo vimekabidhiwa leo Oktoba 12, 2023 jijini Zanzibar na Afisa Habari na Uhusiano wa NHC, Domina Rwemanyila kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo,Abdalah Haji.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, Bi.Rwemanyila amesema, vifaa tiba hivyo vinajumuisha floor meter, patients stand monitor, patients monitor, pulse oximeter, breathing system za anesthetic machine na patients screen.

Katika hatua nyingine,Bi.Rwemanyila amesema, shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kutoa huduma za CSR kwa makundi mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, Majanga na vikundi vya watu wenye mahitaji maalumu ambavyo vinajumuisha watu wenye ulemavu na watoto yatima nchini.

“Tumetoa vifaa hivi, ikiwa ni sehemu ya kurudisha faida tunayoipata kwa jamii ambapo tunatoa huduma pia kwa jamii na tunasaidia pia makundi maalumu, kwa hiyo tukaona tutoe pia kwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar ambao walituomba baadhi ya vifaa.
“Kwa hiyo tumekuja kukabidhi vifaa hivyo leo, ikiwa leo ni zamu ya Zanzibar, na hii ni katika kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa sababu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari na imekuwa ikishirikiana na taasisi na mashirika mbalimbali katika kushiriki shughuli za maendeleo.

“Hivyo na sisi kama NHC tukaona ni vema tukaja kutoa msaada wetu huku ili kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi za kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo Sekta ya Afya ili kuwaletea wananchi maendeleo,”amefafanua Bi.Rwemanyila.

Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.45 ya mwaka 1962.NHC baadae liliunganishwa na iliyokuwa Msajili wa Majumba kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 1990 ambayo ilirekebishwa mwaka 2005 ili kulifanya shirika lijiendeshe lenyewe kibiashara.

Malengo ya shirika kwa mujibu wa Mpango Mkakati wake (2015/16-2024/25) ni pamoja na kuwa msimamizi mahiri wa miliki, kuimarisha uwezo wa kiuendeshaji na udhibiti, kutumia kikamilifu rasilimali watu, kuwa kiongozi katika uendelezaji miliki, kuhuisha mikataba na mazingira ya kisheria na kujenga taswira ya shirika nchini.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo,Haji kwa niaba ya uongozi wa hospitali na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuendelea kuonesha mshikamano mkubwa kwa hospitali hiyo.

Amesema, vifaa tiba hivyo vitasaidia kupunguza changamoto ya awali ambayo ilichangia kuwa na uhitaji hospitalini hapo ili kuweza kutoa huduma kwa ufanisi.

Haji amesema, hospitali hiyo imekuwa ikihudumia wananchi wengi visiwani hapa ikizingatiwa kwamba,hiyo ni taasisi ya umma ambayo inatoa huduma za kitabibu kwa wananchi visiwani Zanzibar.

Pia, amesema Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja jijini Zanzibar imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na taasisi za Serikali na binafsi katika kufanikisha utoaji huduma bora za kitabibu kwa wananchi wote.

Kuhusu MRH

Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ilianzishwa mwaka 1955 na kuitwa Hospitali ya Hassanali Karimjee Jivangee.

Baada ya Mapinduzi ya 1964, Hospitali ya Karimjee ilibadilishwa jina na kuitwa Hospitali ya V.I.Lenin na baadaye kuitwa Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Mwaka 2014, Hospitali ya Mnazi Mmoja ilipandishwa hadhi na kuwa idara miongoni mwa idara za Wizara ya Afya Zanzibar.

Mwaka 2016, Sheria ya Hospitali ya Mnazi Mmoja ilipitishwa na Baraza la Wawakilishi na kutiwa saini mwezi Julai, 2016 na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohammed Shein.

Sheria hiyo inaitambua hospitali hiyo kuwa ni wakala wa Serikali na kuipandisha hadhi na kuwa hospitali ya rufaa na kupewa uwezo wa kuanzisha idara na baadhi ya huduma kwa mujibu wa sheria.

Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita Hospitali ya Mnazi Mmoja iligeuzwa kuwa hospitali ya kisasa ambapo huduma za kitaalam zinatolewa ni pamoja na upasuaji wa mishipa ya fahamu, huduma za Oncology, Dialysis, dharura, na huduma za wagonjwa mahututi na nyinginezo.

Hospitali ya Mnazi Mmoja inatambulika na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa kituo cha kufundisha wahitimu na wafanyakazi wa shahada ya uzamili.

Pia, hospitali imeidhinishwa na COSECSA kama mahali ambapo madaktari wa upasuaji wa jumla na wa neva wanaweza kufunzwa.

Hospitali pia imeidhinishwa na SADCAS katika kutoa vipimo vya maabara. Uongozi na wafanyakazi hujitolea kutimiza maono ya hospitali ya "Kuwa kituo cha ubora cha kutoa huduma ya afya ya kina na nafuu katika Afrika Mashariki".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news