NI SHILINGI NA RUPIA, HII NI MBINU MPYA

NA LWAGA MWAMBANDE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi wamekubaliana kuongeza matumizi ya fedha za nchi kwa maana ya shilingi ya Tanzania na Rupia ya India.

Ni badala ya fedha za kigeni kwenye biashara kati ya mataifa hayo mawili. Hatua hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya dola za Marekani kwenye nchi hizo.

Waziri Mkuu Modi amesema lengo la hatua hiyo ni kuongeza biashara na kupunguza gharama. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, hii ni moja ya mbinu mpya ya kupunguza gharama. Endelea;


1. Ni Shilingi na Rupia, Tanzania na India,
Tutazidi kutumia, biashara kufanyia,
Wao watatupatia, nasi kuwarudishia,
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

2. Rais wa Tanzania, na PM wa India,
Hayo wameyafikia, fedha zetu kutumia,
Vile katika dunia, dola za kugombania
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

3. Hii kweli bora njia, yafaa changamkia,
Bidhaa kihitajia, ili kujinunulia,
Zile tutazotumia, na wanazozitumia,
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

4. Biashara na India, inazidi jipandia,
Fedha zetu kutumia, ni wazi itazidia,
Hakuna kusingizia, dola kujitafutia,
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

5. Pongezi twapatia, hili kusisitizia,
Kwa Shilingi na Rupia, kwenye soko kuingia,
Hii itasaidia, kipindi tunapitia,
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

6. Rais wetu Samia, nawe Modi wa India,
Hili kuliafikia, kwa kweli linavutia,
Tena laweza changia, thamani kuinukia,
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

7. Kikomo tunafikia, cha dola kufukuzia
Hapa kwetu Tanzania, hata nchini India,
Wahindi Watanzania, fedha zao tatumia,
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

8. Fursa changamkia, Shilingi ukitumia,
Bidhaa kununulia, za kuingia India,
Hata Rupia tumia, biashara Tanzania,
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

9. India na Tanzania, mbali tulikoanzia,
Kwake Nyerere anzia, na Indira Gandhi pia,
Kwao tunajipatia, vingi vinavyovutia,
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

10.Na wao kwa Tanzania, mazao wajipatia,
Na miradi mingi pia, Wahindi watufanyia,
Maji na TEHAMA pia, kwao twajifaidia,
Ni moja ya mbinu mpya, ya kupunguza gharama.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news