Polisi wamuokoa Mwanamke aliyetekwa kwa siku nne Dar, watuhumiwa saba wakamatwa

NA GODFREY NNKO

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa saba kwa tuhuma za kupanga njama, kumtishia kwa silaha, na baadae kumteka mwanamke aliyefahamika kwa jina la Hani Nooh Hussein (29) mkazi wa Masaki jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 30, 2023 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Muliro J. Muliro wakati akizungumza na wanahabari.

Amesema, tukio hilo limetokea Oktoba 16, 2023 majira ya saa nne asubuhi wakati Bi. Hani Nooh Hussein akiwa anaendesha gari lake namba T.333 CHN Toyota Rav4.

"Ghafla akiwa eneo la Msasani Village alisimamishwa na sehemu ya kundi la watuhumiwa hao na kuingia ndani ya gari, kumtishia kwa silaha,kumteka na kuelekea maeneo ya Mbezi Beach mtaa wa ujirani ambako walimshikilia kwa nguvu kwa siku nne huku wakidai pesa kwa vitisho kwa baba wa mhanga kuwa asipotoa kiasi cha dola za kimarekani milioni 3.5 mtoto wake atapotezewa maisha."

SACP Muliro amesema, Jeshi la Polisi mara baada ya kupata taarifa ya tukio hilo lilifanya kazi ya ziada ya ufuatiliaji wa kisayansi na Oktoba 19, 2023 Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumuokoa mhanga na kuwakamata watekaji wote wakiwa na gari walilomteka nalo pia silaha iliyotumika Pistol Glock 19 yenye namba LZB 614 iliyotengenezwa Austria ikiwa na risasi nne.

Amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Hassan AbusherNur (39) raia wa Canada mwenye asili ya Somalia, mkazi wa Msasani,Nathan Lungumisa (27),Fredick Chahonza (49), Assad Abdurasur (43),Fahad Mussa (32),Ilfan Saleh (41) na Nicolas Nilay (39).

Kamanda huyo amesema, Jeshi la Polisi limekamilisha upelelezi wa tukio hili na leo Oktoba 30, 2023 watuhumiwa wote watafikishwa Mahakama ya Kisutu kwa hatua zaidi za kisheria.

"Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea kutoa onyo na kuwa halitosita kuchukua hatua za haraka kwa mtu au kundi lolote linalopanga au kujihusisha na vitendo vya kihalifu."

Pia, jeshi hilo limeomba wananchi kuendelea kuchukia uhalifu na kutoa taarifa za wahalifu kwa Jeshi la Polisi ili ziweze kufanyiwa kazi haraka kabla ya matukio.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news