Serikali kuja na mwarobaini wa migogoro ya vigingi na mipasuko Geita

GEITA-Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali itakuja na muafaka na utatuzi wa migogoro ya vigingi na mipasuko kati ya Wakazi wa baadhi ya Mitaa katika Halmashauri ya Mji Geita na Mgodi wa Geita Gold Mine Limited (GGML).
Amesema hayo Oktoba 12, 2023, wakati akizungumza katika mikutano ya hadhara yenye lengo la kusikiliza malalamiko ya wananchi wa mitaa hiyo waliopo ndani ya vigingi vya Mgodi wa GGML.

Mitaa hiyo ni pamoja na Mgusu, Manga, Nyakabale, Mazingamano, Samina, Ikumbayaga, Compaund, Katoma, na Nyanza.
Amesema kuwa baada ya kusikiliza hoja za pande zote za migogoro hiyo ambazo ni kamati inayowakilisha wananchi, wananchi wenyewe, Wamiliki wa leseni ya Uchimbaji yaani Kampuni ya GGML Serikali itakuja na muafaka wa kumaliza tatizo hilo katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja kuanzia sasa.

Mhe. Mavunde amesema kuwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha suala la migogoro hiyo linatatuliwa kwa wakati ili kuwaruhusu wananchi waendelee na shughuli zao za uzalishaji na maendeleo.
“Ndugu zangu, nimechukua maoni yenu na tunakwenda kukaa kikao cha mwisho cha Serikali, GGML na nawaahidi hapa kwa ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa nitaleta mrejesho wa msimamo wa Serikali yetu na majibu mliyosubiria kwa muda mrefu ili kumaliza migogoro hiyo iliyodumu tangu mwaka 2000.

"Nina imani kama mmesubiri kwa zaidi ya miaka 23, basi hamtashindwa ndani ya mwezi mmoja,”amesema Mhe. Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa msingi wa hatua kubwa iliyofikiwa mpaka sasa ni kazi nzuri ya mtangulizi wake, aliyekuwa Waziri wa Madini ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwa kuwa alifanyiakazi maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba amemrahisishia kazi na kwamba Serikali inaenda kumaliza changamoto hiyo baada ya kudumu kwa miaka kadhaa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Geita, Martine Shigella amempongeza Waziri Mavunde kwa kutenga muda wa kuja kusikiliza malalamiko ya wananchi hao licha ya kuwa alishakutana na Kamati inayowawakilisha na kuchukua mapendekezo yao.

Amesema kuwa wakazi hao wamesubiri kwa muda mrefu kupata muafaka wa changamoto zinazowakabili na kwamba hatua iliyofikia italeta faraja kwa wakazi wa mitaa yote yenye migogoro ya vingingi na mipasuko ndani ya Halmashauri ya Geita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news