Mabaharia Tanzania kutambulika zaidi kimataifa

LONDON-Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), imeendelea na juhudi za kuwafungulia fursa mabaharia wa Tanzania kimataifa.

Juzi, kwa niaba ya Serikali TASAC ilisaini Hati ya Makubaliano (MOU) na nchi ya Barbados ili nchi hizo mbili ziweze kutambua vyeti vya mabaharia wa kila upande. Tanzania kwa sasa imesajili vyeti 17,689 vya mabaharia.

Mkurugenzi Mkuu na Msajili wa Mabaharia na Meli wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge pamoja na Msajili Mwandamizi Mkuu wa Mabaharia na Meli wa Barbados Bw. Giovanni Ciniglio wakitia saini Hati ya Makubaliano (MOU) ya kutambuliana vyeti vya mabaharia kati ya nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Barbados jijini London, Uingereza katika ofisi za Ubalozi wa Barbados.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC na Msajili wa Mabaharia na Meli nchini Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge amesema hadi sasa Tanzania imeanzisha mawasiliano na majadiliano na nchi 34 kwa ajili ya kuingia katika makubaliano ya kutambuliana vyeti vya Mabaharia (Memorandum of Understanding – MoUs).

Lengo ni ili kufungua fursa ya ajira kwa mabaharia wetu, lakini pia kuondoa usumbufu wa kushushwa kwa mabaharia wa kitanzania katika meli mbalimbali ambazo zimesajiliwa na nchi ambazo Tanzania haina mkataba nazo.

Barbados ni nchi ya Kisiwani katika Bahari ya Carribean takribani kilomita 430 Kaskazini-Mashariki mwa Venezuela, mpaka sasa ina usajili wa wazi na masharti nafuu (open registry) wa meli 400.

Nchi jirani za karibu kuvukia bahari ni Saint Lucia na Saint Vincent upande wa Magharibi, Trinidad na Tobago upande wa Kusini na Grenada upande wa Kusini-Magharibi.

Mkurugenzi Mkuu na Msajili wa Mabaharia na Meli wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge (kushoto) akiwa na Msajili Mwandamizi Mkuu wa Mabaharia na Meli wa Barbados, Bw. Giovanni Ciniglio mara baada ya wawili hao kusaini Hati ya Makubaliano (MOU) kwa niaba ya nchi zao ili kuruhusu kutambuliwa vyeti vya mabaharia katika nchi hizo. Hafla hiyo ilifanyika juzi katkka ubalozi wa Barbados jijini London, Uingereza. (Picha kwa hisani ya TASAC).
 
“Barbados ni moja ya nchi ambazo tulikuwa tumeanzisha mazungumzo kuhusu kutambuliana vyeti na tunashukuru leo hii tumefanikiwa kusaini Hati ya Makubaliano ya kutambuliana vyeti vya mabaharia, hivyo basi, ni dhahiri kuwa sisi tunatambua mabaharia wa Barbados na wao wanatambua mabaharia wetu,"amesema Bw. Mkeyenge.

Nchi nyingine ambazo Tanzania imeshaanzisha mawasiliano na majadiliano ni pamoja na Bahamas, Algeria, Korea ya Kusini, China, Comoros, Cyprus, Misri, Ufaransa, Ghana, India, Iran, Kenya, Liberia, Malta, Marshall Islands, Mongolia, Oman, Palau, Panama, Peru, Qatar, Saudi Arabia, Singapore, Africa Kusini, Sycheles, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Vanuatu, Vietnam na nchi za Umoja wa Ulaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news