TARURA YAUNGANISHA WANANCHI WILAYANI MOMBA

SONGWE-Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe wameunganishwa baada ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kukamilisha ujenzi wa kivuko cha waenda kwa miguu katika mto Nyamba chenye urefu wa mita 115 na kuunganisha Kata za Ivuna na Mkomba kuelekea Wilaya ya Songwe.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Momba, Mhandisi Yusuph Shaban amesema kuwa kivuko hicho cha waenda kwa miguu ambacho kimegharimu kiasi cha Shilingi milioni 207 kimeweza kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwani sasa wananchi wataweza kuvuka katika kipindi chote cha mwaka na ameeleza kuwa mpango wa TARURA katika Wilaya hiyo ni kuhakikisha linajengwa daraja la kudumu litakalokuwa na uwezo wa kupitisha mizigo."
"Eneo hili lilikua ni changamoto kwa wananchi maana kuvuka upande wa pili ilikuwa vigumu hasa kipindi cha masika lakini sasa kivuko hiki kimekuwa mkombozi na tuna mpango wa kujenga daraja la kudumu litakalopitisha mizigo ili wananchi wa meneo haya waweze kusafirisha mazao yao, kuna mazao kama alizeti, ufuta, mtama na mazao mengine yanayotakiwa kutolewa mashambani na kupelekwa sokoni," amesema Mhandisi Yusuph.

Kwaupande wake Diwani wa Kata ya Ivuna, Mhe. Erick Mkamba amesema kuwa daraja hilo limekuwa muhimu kwani wananchi sasa wanaweza kuvuka na kuzifikia huduma za kijamii kiurahisi na ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea daraja hilo.

“Tunapongeza jitihada za Serikali kupitia TARURA kwa ujenzi wa kivuko hiki ambapo wananchi wanavuka upande wa pili kwa urahisi, ombi langu kwa Serikali ni kujenga daraja la kudumu la moja kwa moja kwani maeneo haya kuna mazao mengi."

Naye Bi. Honorata Emily, Mkazi wa Kijiji cha Ivuna ameishukuru Serikali kwa kuwajengea kivuko hiko kwani hapo awali wananchi walikuwa wanapata shida kuvuka kutokana na maji mengi kujaa hasa kipindi cha mvua na kusababisha akina mama wengi kujifungulia njiani na pia hata wanafunzi walishindwa kuvuka kwenda shuleni.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea kiteputepu wengi tuliumia sana mto ukijaa wiki mbili hadi tatu tulikuwa hatuvuki kwenda kufanya kazi, akina mama tukikuta mto umejaa kujifungua ilikuwa ni shida, pia hata wanafunzi walishindwa kufanya mitihani wengi walifeli kwasababu ya mto huu kujaa maji, tunaishukuru sana Serikali kwa kujenga kivuko hiki ambapo sasa tunavuka kwa urahisi,”amesema Bi. Honorata.

Bw. Leonard Kitwela Mkazi wa Ivuna ameishukuru Serikali kwa kuwajengea kivuko hiko kwani kitawasasaidia kusafirisha mazao yao sokoni na kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news