TARURA yawaunganisha wananchi Wilaya ya Ruangwa na Liwale

LINDI-Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Lindi imekamilisha ujenzi wa daraja la Mbwemkuru lenye urefu wa mita 75 na kufungua barabara ya Ruangwa-Nangurugai- Kiangara-Mirui-Mbwemkuru yenye jumla ya kilomita 65.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Mashaka Narubi ameeleza kuwa kukamilika kwa daraja hilo imekua ni fursa kwa wananchi kusafiri kwa urahisi kutoka Ruangwa kwenda Liwale.

"Daraja hili ni muhimu kwa wananchi wa wilaya zote mbili katika kusafiri na kusafirisha bidhaa na mazao, tumejenga daraja na kufungua barabara na sasa magari yanapita hapa kwenda Liwale," amesema mhandisi Narubi.

Naye, Bi. Sharifa Majaliwa mkazi wa Kijiji cha Nangurugai amesema kuwa kabla ya kujengwa Daraja hilo ilikuwa vigumu kwao kufanya shughuli za kilimo ng'ambo ya pili ya mto lakini kwa sasa wanavuka na kufanya kazi zao kwa urahisi.

"Kutoka hapa Nangurugai kwenda Mirui ilikua ni vigumu, mto una mamba na tulikua tukivuka kwa kutumia njia hatarishi lakini sasa tunashukuru Serikali kwa kukamilisha daraja hili,"amesema Bi Sharifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mirui, Bw. Chande Ally amesema kuwa mwanzoni Kijiji hicho kilikuwa hakifikiki kwani mtu alikuwa hawezi kutoka Mirui kwenda Ruangwa kwa urahisi.

"Kijiji chetu kilikua Kisiwani, ufunguzi wa barabara hii na kukamilika kwa daraja la Mbwemkuru limefungua fursa kubwa za kiuchumi na kijamii,"amesema Bw.Chande.

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inaendelea kufungua barabara katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwezesha wanachi kufika kusikofikika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news