Hazina ya nguzo za asili (natural pillars) zagundulika Hifadhi ya Taifa Ruaha

NA JACOB KASIRI

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika kuongeza mazao mapya ya utalii, hivi karibuni wamegundua eneo jipya lenye hazina kubwa ya Nguzo za Asili (Natural Pillars) zenye muonekano wa kuvutia ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Nguzo hizi zilizosimama mithili ya uyoga na kuvutia kwa macho zinasemekana zimetokana na kulika (kumomonyoka) kwa miamba yenye sifa tofauti kunakosababishwa na mwenendo mzima wa mtiririko wa maji na wakati mwingine pia zikichagizwa na upepo.
Kwa muonekano wa nguzo hizi na jinsi zilivyopangika utadhani kuna Mhandisi kazitengeneza na kuzinakshi, cha kustaajabisha zaidi tabaka la juu lina mwamba mgumu mithili ya kichwa cha binadamu na chini ni kama zimeshikiliwa na mizizi zisianguke, chini ya nguzo hizo pia kuna utitiri wa nguzo ndogo ndogo zinazoendelea kumea na kuongezeka kimo kadri siku zinavyoendelea.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Godwell Meing’ataki, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema, "kwa mara ya kwanza tukiwa tunashuka na Helikopta katika eneo hili, tulishangazwa na wingi wa nguzo hizi za asili (Natural Pillars) na tukajua ndio hazina pekee iliyopo hapo, lakini tulipolizunguka eneo hili tuligundua lina utajiri mwingine wa masalia ya Zana za Mawe mithili ya zile zilizotumika nyakati za Zama za Mawe za Mwanzo".
Zana zinazoonekana katika eneo hilo jipya ni pamoja na mawe magumu yaliyotumiwa na binadamu wa mwanzo kusagia nafaka kwa ajili ya chakula au mizizi na magome ya miti kwa ajili ya tiba asilia, miamba iliyochongwa kiustadi mithili ya mikuki, mashoka na zana nyingine zilizotumika katika shughuli za uwindaji.

Kwa mgeni mwenye kumbukumbu na ufahamu wa Nguzo za Asili (Natural Pillars) na zana za mawe zilizopo Tanzania anaweza kusema hapo ni Isimila, la hasha! ni moja ya eneo lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha takribani kilometa 70 kutoka Makao Makuu ya hifadhi hiyo yaliyopo Msembe.
Aidha, Kamishna Meing'ataki alisema, "kwa utajiri wa nguzo, zana za mawe pamoja na sifa nyingine kedekede eneo hili linakidhi vigezo vya kuwa Geopark, kama tunavyofahamu Bara letu la Afrika lina Geopark mbili tu lakini tunashukuru ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha tuna eneo linaloweza kukidhi vigezo hivyo, likikidhi vigezo litatoa fursa kwa hifadhi hii kutambulika zaidi kimataifa tofauti na ilivyo sasa".

Jitihada za kulitangaza eneo hili zimeanza ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ili kuvutia watalii wengi zaidi na wawekezaji, ukizingatia kuwa hiki ni kivutio kipya na muhimu kwa watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha na hifadhi nyingine zilizoko Ukanda huu wa Kusini.
Kamishna Meing'ataki alisema, "Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) litafanya taratibu za kuwaalika watafiti mbalimbali wa miamba, udongo na Malikale (Archiolojia) wa ndani na nje kubaini na kupata taarifa sahihi za malikale zilizopo, taarifa ambazo zitalitambulisha eneo hili kimataifa".
Aidha, kutokana na unyeti wa eneo hili Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Ruaha imefanya jitihada za kutengeneza barabara ili eneo hilo lifikike kiurahisi hasa kipindi hiki ambacho watalii wengi wanashauku na bashasha ya kwenda kulitembelea na kuziona nguzo na zana hizo.
"Uimarishaji wa barabara unaenda sambamba na tathmini za kiutalii, kiikolojia na kiulinzi kubaini maeneo muhimu yatakayojengwa miundombinu ya kiutalii ili wageni wanapolitembelea eneo hilo wapate huduma ya malazi na chakula. Hatua hizi zikikamilika zitavutia watalii wengi na siku za kukaa hifadhini zinatarajia kuongezaka, siku zikiongezeka na mapato yanaongezeka kwa taifa", alisema Meing’ataki.
Eneo hilo limegunduliwa na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na kupewa jina la "Ruaha Magic Site" tofauti na hapo awali lilikuwa likijulikana kama "Magda", "Ruaha Magic Site" inasadifu zana nzima ya utalii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news