Waziri Dkt.Jafo akutana na wawakilishi wa mashirika ya Kimataifa ya miradi ya mazingira

DAR ES SALAAM-Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo akisalimiana na Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Bi. Clara Makenya muda mfupi kabla ya kuanza kwa kikao baina yake na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam leo Jumatatu (Oktoba 9, 2023). 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Jumatatu (Oktoba 9, 2023) katika Ofisi ndogo za Ofisi Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo alipokea taarifa kutoka kwa wawakilishi hao kuhusu uwasilishaji wa andiko la taarifa la vipaumbele miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi itakayowasilishwa katika Baraza la Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) mwishoni mwa mwezi huu.

Waziri Jafo amesema kikao hicho na wawakilishi wa mashirika hayo sehemu ya ufuatiliaji wa maadhimio ya Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia – GEF, uliofanyika katika Mji wa Vancouver nchini Canada ambapo ambapo nchi zilizoendelea na zinazoendelea zilikubaliana kuwezesha ukusanyaji wa fedha katika shughuli za uhifadhi wa mazingira duniani.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema Tanzania bado ina mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kutoka GEF kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo mara baada ya kumalizika kwa kwa mkutano huo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kupitia vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa ajili ya uratibu wa maombi ya fedha za utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo.

“Tanzania ni mhanga mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Leo ukitazama Wilaya ya Simanjiro utaona ni kwa jinsi gani wafugaji wanavyohangaika na mifugo ya….Si hapo tu na Mpwapwa napo hali nayo si nzuri…Hivyo tunahitaji miradi mingi zaidi ya ufadhili wa fedha ili kuzinusuru jamii zetu” amesema Waziri Jafo.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais, masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi ameyashukuru mashirika hayo kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya mazingira hapa nchini na kuongeza kuwa mahitaji makubwa zaidi ya fedha bado yanahitaji ili kuleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Akitolea mfano Dkt. Muyungi amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali mradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ujenzi wa mradi wa kingo za bahari ya Hindi katika maeneo ya barabara ya Barack Obama (Ocean Road) ambao umelenga kuzuia mmomonyoko wa udongo baharini.

Dkt. Muyungi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya kimataifa ili juhudi za pamoja ziendelee kuimarishwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inaendelea kuibuliwa katika jamii.
Mshauri wa Rais, masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi akibadilishana mawazo na mmoja wa wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao kilichoitishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo Jijini Dar es Salaam leo Jumatatu (Oktoba 9, 2023).

Kwa upande wao wawakilishi wa mashirika hayo wameihakikishia Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa maandalizi muhimu ya uwasilishaji wa taarifa za vipaumbele vya miradi ya mazingira inayosimamiwa na GEF imekamilika na kwa pamoja wameishukuru Serikali kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanya katika kushirikiana na wadau.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Bi. Clara Makenya amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha juhudi za pamoja zinaendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ufadhili wa miradi na uwezeshaji wa fedha.

“Katika andiko letu UNEP tutakalowasilisha GEF tumeainisha maeneo mapya ya miradi kwa Tanzania…Tayari tuna miradi katika maeneo matano…Tumepanga kuangalia awamu ijayo tuanze kuitekeleza Zanzibar na maeneo ya Mikoa ya Nyanda za Juu kusini” amesema Bi. Makenya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akizungumza jambo wakati wa kikao baina yake na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi hapa nchini. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi ndogo za Ofisi ya Makamu wa Rais zilizopo Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam leo Jumatatu (Oktoba 9, 2023).

Mashirika yaliyohudhuria kikao hicho kilichoitishwa Mhe. Waziri Jafo ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambapo mashirika hayo yanafadhili miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Miradi inayofadhiliwa na mashirika hayo ni pamoja na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia (EBARR) na Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news