Waziri Kairuki ataja mafanikio lukuki ya Rais Samia kwenye Sekta ya Utalii

NA JOHN MAPEPELE

SERIKALI imesema inakusudia kukuza utalii wa fukwe, mikutano pamoja na utalii wa kuvinjali kwa meli ikiwa ni mkakati wa kuongeza mazao mapya ya utalii nchini kwa ushirikiano baina ya Tanzania bara na visiwani.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Saba ya Swahili International Tourism Expo - S!TE, 2023 jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema Serikali itaendelea na jitihada za kufikia lengo la kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuweka mazingira wezeshi ya kufikia lengo hilo

Amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais kwa kuwa kinara namba moja wa kukuza sekta ya utalii nchini.

Aidha, amesema Serikali inatambua wajibu huo na imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha uwepo wa mazingira yatakayopelekea- utalii endelevu (sustainable Tourism).

“Ni kwa sababu hiyo Ripoti ya Baraza la Utalii na Masuala ya Safari Duniani (World Travel and Tourism Council, WTTC) ya Mwezi Mei, 2022, imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 Bora Duniani kwa uhimilivu wa maeneo yake kupokea watalii (sustainability). Matunda ya hatua zinazochukuliwa na Serikali yanaonekana wazi. Leo hii pamoja na athari za UVIKO19, tunafurahi kwamba, kasi ya kukua kwa sekta ya utalii wetu ni nzuri,”amefafanua Mhe.Kairuki.

Waziri Kairuki ameongeza kuwa mafanikio hayo yamepelekea, Sekta ya utalii kuchangia asilimia 25 ya fedha za kigeni, na asilimia 17.5 ya pato la taifa ambapo amesisitiza kuwa huo ni mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi yetu.

Amesema sekta ya utalii inatoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa wananchi na kwamba Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba sekta hii inabaki kuwa imara, na inazidi kukua.

Pia amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu kama vile barabara, reli na viwanja vya ndege ili kuhakikisha wageni wanayafikia maeneo yote yenye vivutio vya utalii kwa urahisi.

Amesema, Serikali imeendelea kuliimarisha zaidi Shirika letu la Taifa la ndege la “Air Tanzania” (ATCL) ili kuimarisha usafiri wa anga ambapo amesema katika siku za hivi karibuni ATCL limeanza safari za moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda India, China na nchi za jirani ambapo mwakani linatarajia kuanza safari zake barani Ulaya.

Amesisitiza kwamba, kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa, mashirika mbalimbali ya kimataifa yaliyokuwa yamesitisha safari zao wakati wa kipindi cha UVIKO19 yamerejesha safari zao za kuja nchini na mashirika mengine kama Air France, Saudi Airlines, yameanza safari mpya za kuja Tanzania, pia mashirika megine mengi yameanzisha safari maalum “Charted Flights” kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja nchini.

“Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mazingira ya biashara nchini, ili kuvutia uwekezaji nchini kwenye sekta mbali mbali, ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii. Ni dhahiri kuwa kwa namna ya pekee kabisa, sekta ya utalii inategemea sana mchango wa sekta binafsi, hasa kwenye ujenzi na uendeshaji wa mahoteli, na kwenye huduma za usafiri. Ni kwasababu hiyo katika Maonesho ya Mwaka huu pamoja na mikutano ya kibiashara kutakuwa pia na Mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji.” amefafanua Mhe. Kairuki.

Amesema Serikali kupitia Wizara yake itaendelea kufanya jitihada za kufungua maeneo mengine ya nchi yetu kwa ajili ya utalii, kwa sababu Tanzania ina vivutio vya kutosha katika mikoa yote. Pia itaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa “REGROW” kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, kwa ajili ya kukuza utalii katika eneo la Nyanda za Juu Kusini. Pia ametoa wito kwa Viongozi wa Mikoa na sekta binafsi kushirikisha kikamilifu kutangaza vivutio katika kanda zote nchini.

Vilevile, amesema Serikali itaendelea kuyaimarisha na kuyaboresha matamasha mbalimbali yanayofanyika nchini ili yafikie viwango vya kimataifa na kwamba dhamira ya Serikali ni kuona matamasha yake yanaingia kwenye kalenda za dunia za utalii, na hivyo kuongeza idadi ya watalii hapa nchini.

Juhudi kubwa pia zinafanyika kwa kutangaza utalii wetu nje ya nchi kupitia ushiriki wa maonesho ya kimataifa kwenye nchi mbalimbali, na kupitia road shows zinazoandaliwa na Serikali yetu. Juhudi hizi zimeanza kuzaa matunda.

Amezipongeza sekta binafsi kwa umahiri wake wa kusaidia kutangaza utalii na kwa kutoa huduma nzuri ambayo imesaidia kuitangaza nchi. Pamoja na balozi zote zilizo nje ya nchi kwa kufanya juhudi kubwa za kuvutia watalii kuja hapa nchini pia Balozi za Nje zilizopo nchini kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa wa kuitangaza Tanzania katika nchi zao.

Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Simai Said kutoka Zanzibar amesema Serikali yake itashirikiana kikamilifu katika kuimbarisha utalii hususan utalii wa fukwe ambapo pia ameshauri kuboreshwa kwa tozo mbalimbali kwenye sekta ya utalii.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Timotheo Mzava amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kuboresha utalii nchini na ameshauri kufufua mazao mapya ya utalii, kufungua maeneo maeneo ya kusini na kuunganisha utalii wa Tanzania bara na visiwani.Maonesho ya S!TE ya mwaka huu yamehusisha waoneshaji zaidi ya 150 na wanunuzi wa kimataifa wapatao 100 wanaotoka nchi mbali mbali duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news