Waziri wa Fedha awahoji wanaosema fedha zinaibiwa

DAR ES SALAAM-Waziri wa Fedha,Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema, kuna watu wanaosema katika kipindi hiki fedha zinaibiwa na kwamba yeye ana swali moja kwao ya kwamba kama fedha zinaweza zikaibiwa, lakini bado kukawa na maendeleo kwenye sekta mbalimbali nchini, Je? Wakati haziibiwi, zilikuwa zinaenda wapi?.

Dkt. Mwigulu amehoji swali hilo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu leo wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya Mwaka 2022 na Ugawaji wa Magari ya Kubebea Wagonjwa na Vifaa Tiba jijini Dar es salaam.

"Mheshimiwa Rais niseme machache, moja ya kazi unazozifanya Mheshimiwa Rais inaiheshimisha Tanzania, amesema na Mwenyekiti wa Kamati ametoa tarifa kwamba, hata mataifa mengine mbalimbali wanakuja Tanzania kuja kupata huduma za afya.

"La pili, Mheshimiwa Rais kazi unazozifanya zinakiheshimisha Chama Cha Mapinduzi wewe ukiwa ndiye Mwenyekiti wake,na zinakitofautisha Chama Cha Mapinduzi na vyama vingine. Na la tatu, Mheshimiwa Rais kazi unazozifanya zinautambulisha utu wa mwanamke na utu wa watoto.

"Tutaona kwenye takwimu jinsi ulivyofanya kazi kubwa, katika muda mfupi umefanya maendeleo jumuishi kwamba si tu leo unavyotoa magari, sisi tulio kwenye Sekta ya Fedha huku tunaziona kazi zako.

"Kwamba magari peke yake yasingetosha, Mheshimiwa Rais ukaongeza bajeti ya TARURA kutoka takribani bilioni 200 mpaka zaidi ya trilioni 1.3 ili mgonjwa anapotokea kwenye kijiji chochote aweze kufuatwa na gari majira yote.

"Umetoa magari, lakini umetengeneza barabara zinazounganisha vijiji vyote. Mheshimiwa Rais, siyo hilo tu, umepunguza mwendo ungeweza kuacha tu kwamba umeshapeleka magari kwenda mwendo mrefu, lakini katika kipindi kidogo ambacho umekaa, umejenga vituo tarafa zote za nchi hii na kila kata za kimkakati.

"Na Mheshimiwa Rais, si hiyo tu afya inaenda sambamba na sekta zingine muhimu, umeongeza fedha kwenye upande wa elimu, ngazi zote ili Watanzania waweze kuelimika na wakishaelimika watajali masuala ya afaya kama tulivyoelezewa hapa kuondokana na mila potofu.

"Lakini, si hivyo tu Mheshimiwa Rais, umehakikisha maji safi na salama yanapatikana, umeongeza bajeti ya maji kuliko kipindi chochote kile ili maji yaweze kuendana sambamba na huduma hizo za afya.

“Sasa kwa kuwa walisema aje mtu wa maokoto hapa aweze kutoa ushaidi, niseme tu wale wanaofupisha kazi zako watasema ni kodi zetu.

"Lakini Mheshimiwa Rais kodi zilikuwepo tangu enzi za kodi ya kichwa, ikaja kodi ya mbwa, kodi ya baiskeli na nyinginezo, itoshe tu kusema maelekezo yako ya kusema fedha ziende kutekeleza miradi ya maendeleo ndio matokeo yake haya tunayoyaona katika sekta hizi mbalimbaliu.

“Na wengine wanaosema fedha zinaibiwa, mimi swali limekuwa jepesi tu, kama fedha zinaweza zikaibiwa, lakini bado ukapeleka MRI kote, ukatengeneza vituo vya afya tarafa zote vya kisasa ambavyo vinapatikana kwenye nchi zinazoendelea.

"Ukanunua magari mengi kwa mpigo, Je, wakati haziibiwi? Kwa sababu wewe ni Rais wa Sita, Je wakati haziibiwi zilikuwa zinaenda wapi? Kwa sababu hivi ni vitu vinaonekana na vimenunuliwa kwa fedha.

"Kwa hiyo katika salamu Mheshimiwa Rais itoshe tu kukupongeza na kwa kweli sisi hata tusiposema, kazi hizi unazozitekeleza zinajieleza."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news