Dkt.Msonde:Serikali itamaliza kero za walimu ili wafundishe kwa umahiri

NA JAMES MWANAMYOTO

NAIBU Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt.Charles Msonde amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kumaliza kero zote zinazowakabili walimu nchini ili wabaki na jukumu moja tu la kufundisha kwa umahiri.
Dkt. Msonde hayo mjini Iringa wakati akifunga mafunzo ya walimu mahiri wanaofundisha darasa la awali yaliyokuwa yakifanyika katika Chuo cha Ualimu Klerruu, kwa lengo la kuwapatia ujuzi na maarifa ya kuutekeleza vyema mtaala wa Darasa la Awali.

Amesema, Serikali kwa makusudi imeamua kushughulikia kero zote za waalimu ndio maana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameelekeza waajiri na watendaji wote walio chini yake kuhakikisha wanamaliza kero zote za walimu nchini.

“Mhe. Mchengerwa amesema hataki kusikia mwalimu yeyote nchini analalamika wakati Serikali imedhamiria kutatua changamoto zote zinazowakabili,” Dkt.Msonde amesisitiza.

Kutokana na azma hiyo ya Serikali, Dkt. Msonde amesema walimu wote nchini wanatakiwa kuwa na jukumu la kufundisha tu ili umahiri utokee na tija ipatikane katika eneo la taaluma.

“Tunataka walimu wawe na kazi moja tu ya kuhakikisha mnatekeleza mitaala mipya vizuri ili watoto wapate ujuzi utakaowawezesha kupata ufaulu mzuri na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa hapo baadae,”Dkt. Msonde amehimiza.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kutatua kero za walimu, Dkt. Msonde ameainisha kuwa zoezi la kutatua changamoto utofauti wa upandishaji wa madaraja limeshanyika kwa uratibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu na kuongeza kuwa, changamoto ya madai ya malimbikizo ya mishahara nayo imeshughulikiwa na inaendelea kufanyiwa kazi na Ofisi ya Rais-UTUMISHI.

Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mafunzo ya walimu mahiri wanaofundisha darasa la awali Bi. Sophia Kilavi ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo ya maudhui ya mtaala mpya wa mwaka 2023 ulioboreshwa ambao wanakwenda kuutekeleza.

Bi. Kilavi amesema wamejifunza kwamba katika ufundisha wa watoto wa elimu ya awali wanapaswa kutumia vifaa vya TEHAMA vikiwepo vishikwambi, kompyuta na televisheni ili kuwawezesha watoto kumudu stadi mbalimbali zilizokusudiwa katika mtaala.

Aidha, Bi. Kilavi amesema pia wamejifunza namna ya uchopekaji wa masuala ya mtambuka ikiwemo elimu ya fedha ya fedha ya kitanzania, utu, maadili, imani na utamaduni.

Mafunzo haya kwa awamu ya kwanza yamewahusisha jumla ya walimu 1,832 ambao wamegawanyika katika vituo vitano ambavyo ni Chuo cha Ualimu Kleruu na katika Shule za msingi Gangilonga, Kiesa, Kigambani, na Njia Panda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news