Dkt.Shein aguswa na ufanisi wa Chuo Kikuu Mzumbe

ZANZIBAR-Rais mstaafu wa Awamu ya Saba wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohammed Shein amefurahishwa na taarifa ya maendeleo ya chuo hicho iliyowasilishwa kwake na Kaimu Makamu Mkuu wa chuo, Prof. William Mwegoha siku ya Novemba 8, 2023.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha (kulia) akikabidhi taarifa ya maendeleo ya chuo na maandalizi ya Mahafali ya 22 kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Saba wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkuu wa Chuo, Dkt. Ali Mohammed Shein, mara baada ya kumtembelea ofisini kwake Mazizini jijini Zanzibar.

Katika kuwasilisha taarifa hiyo uongozi wa chuo umeongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la chuo, Prof. Saida Yahya Othman na Kaimu Makamu Mkuu wa chuo, Prof. William Mwegoha ambao wamemtembelea Mkuu huyo wa Chuo kwa lengo la kutoa taarifa ya Maendeleo ya Chuo kwa kipindi cha miezi sita yaani (mwezi Mei - Novemba, 2023)

Prof. Mwegoha amesema,chuo kinatarajia kuanzisha kituo cha mafunzo na mitaala kwa ajili ya Uongozi na Menejimenti (Centre for Leadership and Governance) kwa lengo kutoa mafunzo kwa viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohammed Shein akizungumza na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Saida Yahya Othman pamoja na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, mara baada ya kumtembelea Ofisini kwake, Mazizini-Zanzibar.

Aidha, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, amemtaarifu Dkt. Shein kuhusu udahili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika mwaka wa masomo 2023/2024 na kuanisha kuwa hadi kufikia mwezi Oktoba 2023 wanafunzi waliodahiliwa kwa kozi mbalimbali ni 7887.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha amesema katika mahafali ya 22 ya Chuo yanayotarajiwa kufanyika Mwezi Novemba na Desemba mwaka huu katika Kampasi za Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam jumla ya wahitimu 3943 watatunukiwa Astashahada, Stashahada na Shahada mbalimbali.
“Nafurahi kukutaarifu kwamba kati ya wahitimu hao asilimia 51.46 ni wanawake na asilimia 48.54 ni wanaume,” Mwegoha amefafanua.

Akizungumza na viongozi hao Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkuu wa Chuo, Dkt. Ali Mohammed Shein amefurahishwa na mafanikio ya Chuo na kuwataka viongozi hao kuhakikisha wanatoa msukumo madhubuti katika ujenzi wa hosteli ya wasichana Ndaki ya Mbeya ikiwa ni agenda ya dhati ya kuweka mazingira bora ya kusoma kwa watoto wa kike.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Ali Mohammed Shein, akiwa katika picha ya pamoja na ugeni kutoka Chuo Kikuu Mzumbe. Aliyeketi kushoto ni Prof. Saida Yahya Othman, Mwenyekiti wa Baraza na aliyeketi kulia ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha. waliosimama, kulia ni Mwanasheria wa Chuo, Bi. Eveline Kweka na kushoto ni Katibu wa Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Aloyce Gervas, mara baada ya kumtembelea Ofisini kwake Mazizini, Zanzibar.

“Ujenzi wa Hosteli ni muhimu sana kwa wanafunzi wa kike na takwimu zinaonyesha kuwa ufaulu wa wanafunzi wa kike nchini unaongezeka. Hivyo juhudi za kuendeleza ujenzi wa hosteli ni juhudi zenye maslahi mapana kwa nchi yetu katika kuweka mazingira wezeshi ya kujifunzia,”amesisitiza Dkt. Shein.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news