Meya wa Dar es Salaam ahimiza kujiunga na Bima ya Afya kabla ya kuugua

DAR ES SALAAM-Wananchi wamehimizwa kujiunga na bima ya afya kabla ya kuugua ili wawe na uhakika wa matibabu pindi wanapopata janga la kuugua.

Hayo yamesemwa na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Omary S. Kambilamoto alipotembelea Banda la Mfuko wa Taia wa Bima ya Afya (NHIF) katika Maadhimisho ya Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza inayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.

Akizungumzia hilo aliwataka wananchi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi wiki hii kuja kupima afya zao na kupata elimu ya kujiepusha na magonjwa haya na umuhimu wa kuwa na bima ya afya.

"Magonjwa yasioambukiza yanaepukika endapo kila mtu atazingatia kuishi mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi na kula lishe bora. Aidha, kila mtu azingatue kuwa na bima ya afya ili endapo atapata ugonjwa aweze kutibiwa bila kikwazo,"amesema Mhe. Kambilamoto.

Naye Meneja Uhusiano wa NHIF Bi. Anjela Mziray akitoa maelezo ya huduma zinazotolewa na Mfuko katika maadhimishimo hayo yaliyoanza tarehe 11 na kupangwa kuisha 18 Novemba, 2023 amesema gharama za matibabu kwa magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa hivyo elimu ni muhimu kuendelea kutolewa.

Akitoa takwimu za matibabu ya magonjwa haya amesema kwa wastani gharama za matibabu kwa mgonjwa wa saratani kwa mwaka ni Sh. 69.9 milioni na kwa matibabu ya figo ni Sh. 35.8 milioni kwa mwaka.
Aidha, amesema tathmini za jumla ya malipo ya NHIF kwa matibabu ya saratani yameongezeka kutoka Sh. 12.2 bilioni kwa mwaka 2016/17 hadi Sh. 32.4 mwaka 2021/22. Kwa matibabu ya figo, jumla ya malipo hayo yameongezeka kutoka Sh. 11.4 bilioni mwaka 2016/17 hadi Sh. 35.4 bilioni kwa mwaka 2021/22.

"Takwimu hizi zinaonesha changamoto ya ugharamiaji wa magonjwa haya ni kubwa na elimu ya kujiepusha ni msingi pamoja na watu kuwa na bima ya afya kabla ya kuugua," amesema Bi. Mziray.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news