Mwinjilisti Temba:Simba acheni ulimbukeni, Yanga imewekeza na Kocha arejeshwe hana shida

DAR ES SALAAM-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba ameutaka uongozi wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam kuacha ulimbukeni, kwani kumfukuza Kocha Mkuu si suluhisho la changamoto zinazoikabili klabu hiyo katika kupata matokeo bora uwanjani.

Temba ambaye ni mbeba maono wa Kanisa la Penuel Healing Ministry la Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Redio ya Penuel iliyopo mkoani Kilimanjaro ameyasema hayo wakati akitoa maoni yake kuhusu mustakabali mwema wa soka la Tanzania na uwekezaji katika timu na klabu mbalimbali nchini.

"Nizungumze kitu kimoja kuhusiana na mambo ya mpira, hebu viongozi wa timu ya Simba, viongozi na mashabiki wote wa Klabu ya Simba, tusiwe malimbukeni jamani.

"Sawa,Simba imefungwa, imefungwa goli tano, lakini hebu tuangalie ni mchezaji gani ambaye tulikuwa tunafikiri apangwe, lakini hakupangwa angalau Simba ingefunga, karibu wachezaji wote Simba walipangwa.

"Labda Bocco peke yake, sasa tuje na mjadala kwamba tunamfukuza Kocha kwa sababu hakumuweka Bocco angemuweka Bocco angalau angerusha mabao mawili hata matatu, mimi ninasema hivi viongozi wa Simba ndiyo shida.

"Kwa sababu wanawafanya mashabiki wa Simba kama vile wanawapa keki hivi, yaani Simba imerudi kwenye mambo ya siasa, jamani Simba si imewahi kuifunga Yanga goli tano na zile za Tanga si nane, jamani si mgewakumbusha tu jamani kwamba hii labda ni bahati mbaya?.

"Kwa mara ya kwanza Simba huko kwa Waarabu huko kila mara inaenda kufungwa, kocha huyu huyu mliyemfukuza ndiye aliyeisababisha Simba ikatoa suluhu,hebu mpeni heshima yake, mpeni maua yake.

"Mimi ninawaambia viongozi wa Simba kama mliyokuwa mnayafanya kwa Phiri wa Zambia, mnamfukuza mnamrudisha, huyu mtamrudisha. Mimi ninataka mmrudishe kwa sababu yeye anataka matokeo.

"Simba hii inajulikana kabisa ina shida muda mrefu,hapa hii inaonekana Simba haijawahi kufungwa zaidi ya Yanga, ni kwa sababu ya huyu huyu ambaye aliona madhaifu, huyu ana muda wa mwaka mmoja, mlimpa muda wa kuwachagua wachezaji?.

"Wote aliwakuta, wachezaji wengine, anawatumia hao hao, yeye kazi yake ni kuchagua tu, alimkuta Kibu mfano kila mtu alimchukia, wachezaji wote Simba walimchukia,mashabiki wote Simba walimchukia, akampa zawadi Kibu watu wakashangaa, anampaje zawadi Kibu huyu?.

"Kibu hadi leo karudi Taifa Stars na Kibu huyu amepewa uraia kwa sababu ya kucheza mpira, yaani kitendo tu cha kumsababisha Kibu akarudi kwenye mfumo alikuwa ametoka Taifa Stars akarudishwa, akawa ndiye mchezaji anayetegemewa kufunga, mbona hamkuliona hilo moja, haya mpeni basi mnaye mpa sasa hivi.

"Simba ikifungwa itakuwaje? Je mmewekeza, Yanga wamewekeza mkipata mtu wa kuwasaidia hivyo hivyo muende naye, kwa hiyo viongozi wa Simba wanaleta siasa.

"Mnaleta siasa na wewe Msemaji wa Simba acheni kuleta siasa, yaani kocha hana shida kabisa yaani fundi hana shida kabisa, kwa hiyo ninachoomba mkiona Simba inaporomoka mkampigie magoti mmrudishe aendelee na kazi,"amefafanua kwa kina Mwinjilisti Temba.

Novemba 7,2023 Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imesema, imefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba wa Kocha Mkuu wa Kikosi cha kwanza Roberto Oliveira Gancalves Do Carmo (Robetinho).

Pia, klabu hiyo imefikia makubaliano ya kusitisha mkataba wa kocha wa viungo Corneille Hategekimana amapo katika kipindi chote cha mpito kikosi kitakuwa chini ya Kocha Daniel Cadena akisaidiwa na Seleman Matola.

Uamuzi huo ulifikiwa ikiwa ni siku chache, Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam kuishushia Simba SC kipigo cha mabao 5-1 ndani ya Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini humo.

Katika mtanange huo, Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam ilijikuta katika wakati mgumu kupitia Derby ya Kariakoo baada ya kupoteza kwa mabao 5-1.

Aidha, kupitia Derby hiyo, kikosi cha Yanga kilipata bao la mapema dakika ya tatu kupitia kwa Kennedy Musonda kwa baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Yao Attohoula.

Kibu Denis aliwapatia Simba SC bao la kusawazisha kwa kichwa dakika ya tisa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Said Ntibazonkiza.

Max Nzengeli aliwapatia Yanga bao la pili dakika ya 64 kwa shuti kali la chini chini baada ya kuwazidi ujanja walinzi wetu wa Kati.

Aziz Ki aliwapatia Yanga bao la tatu dakika ya 72 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Clement Mzize.

Nzengeli aliwapatia Yanga bao la nne dakika ya 77 akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi safi ya Mzize. Bao la tano kwa klabu ya Yanga lilipelekwa nyavuni na Pacome dakika ya 87 kwa mkwaju wa penalti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news