Naibu Waziri Kapinga aipongeza REA usambazaji nishati vijijini

VERONICA SIMBA NA LILIAN LUNDO

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ametoa pongezi kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi nzuri ya kuendelea kusambaza umeme pamoja na aina nyingine za nishati vijijini ili kuhakikisha wananchi wote waishio vijijini wanafikiwa na huduma hiyo hivyo kuboresha maisha yao.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (kulia) akimkaribisha Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dodoma, alipofika kuwatembelea na kuzungumza na Menejimenti, Novemba 7, 2023.

Kapinga ametoa pongezi hizo Novemba 7, 2023 wakati akizungumza na Menejimenti ya REA, ikiwa ni kikao chake cha kwanza na Uongozi wa Wakala hiyo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Makao Makuu ya Wakala hiyo, Novemba 7, 2023 ikiwa ni kikao chake cha kwanza pamoja nao tangu aliposhika wadhifa huo.

“Kazi ya REA inafanyika vizuri sana kwakweli. Mimi nimepita huko, kabla hata sijaja ofisini. Miradi mingi inafanyika vizuri sana kwakweli. Kwahiyo niwapongeze, mnafanya kazi nzuri ya kusimamia na hata kubuni miradi. Mambo ni mazuri,” amesema Mhe. Kapinga.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka akizungumza wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kilichofanyika Makao Makuu ya Wakala hiyo jijini Dodoma, Novemba 7, 2023. Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Mhandisi Styden Rwebangila.

Pamoja na pongezi hizo, Naibu Waziri ameishauri REA kuendelea kuwajengea uwezo wasimamizi wa miradi, ili waweze kuifahamu na hivyo kuisimamia vizuri katika hatua zote tangu inavyoanza hadi inapokamilika kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Adrophina Tutuba (kushoto), akimkabidhi Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga, Mfuko wenye baadhi ya zawadi zilizotolewa na Wafanyakazi wanawake wa Wakala hiyo kama pongezi kwake akiwa ni mwanamke mwenzao kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo nyeti. Naibu Waziri alitembelea Makao Makuu ya REA jijini Dodoma, Novemba 7, 2023 na kuzungumza na Menejimenti ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu aliposhika wadhifa huo.

“Nafahamu wengi ni wapya na wako baadhi ni wazuri na wengine siyo wazuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutoijua vizuri miradi, kutokuifuatilia vizuri au uzembe tu, Hivyo nashauri muwajengee uwezo na kuhakikisha wanasimamia miradi kuanzia mwanzo, kwani ndiyo muda sahihi na unaofaa,” amefafanua.

Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage (kushoto), akimkabidhi Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga, baadhi ya zawadi zilizotolewa na Wafanyakazi wanawake wa Wakala hiyo kama pongezi kwake akiwa ni mwanamke mwenzao kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo nyeti. Naibu Waziri alitembelea Makao Makuu ya REA jijini Dodoma, Novemba 7, 2023 na kuzungumza na Menejimenti ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu aliposhika wadhifa huo.

Akieleza zaidi, Mhe. Kapinga amesema aina ya ufuatiliaji unaotakiwa katika miradi ni pamoja na kuhakikisha pesa zinazotolewa kwa Wakandarasi zinatumika kwa matumizi stahiki pamoja na kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa wakati.

Aidha, ameishauri REA kuhakikisha kuwa inajenga mazuri ya miradi inayotekelezwa ili inufaishe jamii kwa kipindi kirefu yaani vizazi na vizazi.

Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao, Novemba 7, 2023. Naibu Waziri alitembelea Makao Makuu ya Wakala hiyo jijini Dodoma ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Akizungumzia suala la uunganishaji wateja katika maeneo ambayo miradi mbalimbali ya umeme imekamilika, Naibu Waziri amesema ni vyema nguvu ya kutosha ikaelekezwa katika kuhakikisha wananchi wanaelimishwa na kuhamasishwa kuunganisha umeme ili miradi hiyo iwe na tija kwakuwa Serikali inatumia fedha nyingi sana kutekeleza miradi hiyo.

Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao, Novemba 7, 2023. Naibu Waziri alitembelea Makao Makuu ya Wakala hiyo jijini Dodoma ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

“Suala la kuunganisha wateja tulichukulie kwa uzito kama ambavyo tunaweka uzito mwingi katika utekelezaji wa miradi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa Wakala unaahidi kuendelea kujituma pamoja na kuleta ubunifu katika kuharakisha upatikanaji wa nishati bora maeneo ya vijijini.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), baada ya kikao baina yao alipotembelea Ofisi za Wakala Novemba 7, 2023. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Athumani Mbuttuka na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy.

Aidha, ameongeza kusema kuwa Wakala utaendelea kupokea maelekezo na miongozo kutoka kwa viongozi wa Wizara ya Nishati na Mamlaka nyingine za Serikali katika kutimiza wajibu wake na kufanikisha malengo na azma ya Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi waishio vijijini kupitia upatikanaji wa nishati bora katika maeneo yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news