Naibu Waziri Kapinga:Wanawake vijana jishughulisheni na ujasiriamali, biashara

MOROGORO-Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, amewataka Wanawake Vijana kujishughulisha na Biashara pamoja na Ujasiriamali ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga (wa pili kulia) akicheza pamoja na Washiriki wa Kongamano la Wanawake Vijana ambao ni Wafanyabiashara na Wajasiriamali wimbo unaoashiria umoja na mshikamano kwa wanawake wakati wa kongamano hilo lililofanyika Morogoro.

Wito huo umetolewa tarehe 11 Novemba 2023 wakati alipofanya ufunguzi wa Kongamano la Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Ladies Talk Tanzania Initiative inayojishughulisha na masuala mbali mbali ya kijamii pamoja na Ujasiriamali lililofanyika mkoani Morogoro.

"Niseme ukweli ya kwamba, ni nia ya dhati kabisa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutaka Wanawake wote nchini na duniani kote kusonga mbele kiuchumi, kuwa walezi wazuri wa familia na viongozi katika Sekta mbalimbali katika ngazi mbalimbali za uongozi."mesema Naibu Waziri Kapinga.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, akizungumza na Wanawake Vijana wanaojishughulisha na biashara pamoja na Ujasiriamali wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Taasisi isiyo ya Kiserikali Ladies Talk Tanzania Initiative inayojishughulisha na masuala mbali mbali ya kijamii pamoja na Ujasiriamali lililofanyika Mkoani Morogoro tarehe 11 Novemba, 2023.

Naibu Waziri Kapinga amewasisitiza, Wanawake Vijana kujishughulisha na ujasiriamali na kushikana mkono pale wanapofanikiwa kufikia hatua fulani ya maendeleo katika biashara na shughuli za Ujasiriamali.

"Ninaamini kabisa, kwa kila mmoja wenu hapa, hatua uliyofikia, kuna mtu alikushika mkono. Hivyo ni muhimu sana kukumbuka, unapoinuka juu kiuchumi, kumbuka kuwashika mkono wengine ambao wanahitaji kutiwa moyo, kuhamasishwa na kuwezeshwa kupiga hatua katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo biashara na ujasiriamali kama shughuli hizi mnazozifanya,"ameeleza kwa hisia Naibu Waziri Kapinga.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga (wa kwanza) akiwa pamoja na Vingozi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Ladies Talk Tanzania Initiative inayojishughulisha na masuala mbali mbali ya kijamii pamoja na Ujasiriamali wakati wa sala ya pamoja kabla ya kuanza rasmi shughuli za Kongamano hilo lililofanyika mkoani Morogoro.

Aidha, Naibu Waziri Kapinga amewataka wanawake vijana kutohofia kuanza kujishughulisha na wazo jipya la kibiashara au ujasiriamali kwa kuhofia kutofanikiwa katika shughuli husika.


"Kijana usiishi ndoto za watu wengine, kile ambacho unafanya ndicho hicho ukisimamie na ufanye kwa bidii na kukipenda. Uanze sasa kwa chochote ulicho nacho haijalishi ni kikubwa au kidogo,"amesema Mhe. Kapinga.

Katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Kapinga amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Ladies Talk Tanzania, Bi. Salome Sengo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusaidia jamii na kutoa elimu ya Ujasiliamali kwa Wanawake Vijana.
Mtendajii Mkuu wa Wakala wa Mbegu (ASA) Dkt. Sophia Kashenge akizungumza wakati wa Kongamano la Taasisi isiyo ya Kiserikali Ladies Talk Tanzania Initiative inayojishughulisha na masuala mbali mbali ya kijamii pamoja na biashara na Ujasiliamali wakati wa Kongamano la washiriki hao lililofanyika Mkoani Morogoro tarehe 11 Novemba. 2023.

Kwa upande wake Mtendajii Mkuu wa Wakala wa Mbegu (ASA),Dkt.Sophia Kashenge amewasisitiza Vijana kuwa na uthubutu katika kujiajiri na kuona ni vitu gani wanaweza kufanya ili kujikwamua kiuchumi, na kufikiria kitofauti kufanya kilimo chenye tija.


Mkurugenzi Mtendaji wa Ladies Talk Tanzania Initiative, Salome Sengo amemshukuru Naibu Waziri Kapinga kwa kuhudhuria hafla hiyo pamoja na kutambua ushiriki na uwepo wa wadau mbali mbali wa Ujasiriamali waliowezesha, kufanikisha kongamano hilo.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga (wa tatu kutoka kulia) akiwa pamoja na Viongozi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Ladies Talk Tanzania Initiative inayojishughulisha na masuala mbali mbali ya kijamii pamoja na Ujasiliamali katika Kongamano la Taasisi hiyo, lililofanyika mkoani Morogoro.

Kongamano hilo la siku moja limeshirikisha Wanawake Vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news