Rais Dkt.Mwinyi aahidi neema zaidi Sekta ya Michezo

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itaimarisha miundombinu ya michezo kote nchini.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa ahadi hiyo leo Novemba 20, 2023 Ikulu jijini Zanzibar alipojumuika kwenye chakula cha mchana na wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15, Karume Boys, baada ya kunyakua kombe la CECAFA nchini Uganda.

Dkt. Mwinyi amesema michezo ni afya, ajira, utalii pia huwaunganisha jamii kwa watu kufurahi pamoja na kuwa kitu kimoja.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema, Zanzibar haitegemei utalii wa urithi pekee unaotokana na hifadhi ya Mji Mkongwe pamoja na fukwe lakini pia michezo ni utalii mkubwa na wakutegemewa.

Amesema, Zanzibar inatarajiwa kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON mwaka 2027 hivyo imejipanga kuimarisha miundombinu ya kisasa kwenye sekta ya michezo pamoja na kushajihisha sekta ya utalii hususani hoteli na nyumba za kufikia wageni.

Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita alisema Wizara ilipewa dhamana na Serikali ya kuisafirisha timu hiyo ambapo Rais Dk. Mwinyi alitoa usafiri wa ndege kwa Karume Boys kama zawadi wakati wa kurejea nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Muhamed Said Dimwa alishauri kupatiwa mafunzo maalumu ya michezo walimu wawili kwa Karume Boys.

Kwa upande wake Rais wa ZFA, Suleiman Mahmoud Jabir alisema mafanikio ya ushindi wa Karume Boys yaliyokana na juhudi na ushirikiano wa wadau wengi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news